BILIONI 1.1 ZATENGWA KUPAMBANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Saada Mkuya leo 28/01/2022 mara baada ya kumtembelea Ofisi kwake. Dkt Jafo amefanya ziara ya siku moja Zanzibar kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini unaotekelezwa Kaskazini A - Unguja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akimsikiliza Bi. Fatma Omar Katibu wa Kikundi cha wajasiriamali Matemwa, kikundi kinachojihusisha na uzalishaji wa vipodozi kwa kutumia rasilimali za misitu. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mahmoud na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Saada Mkuya


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani akipata maelezo ya wataalamu kuhusu hatua za uchimbaji wa visima katika eneo la Matemwe Kijini. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mahmoud, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Saada Mkuya na Mkurugenzi wa Mazingira Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikagua eneo lililoathirika na Mabadiliko ya tabianchi na kuzungumza na wananchi katika eneo la Nungwi. Serikali imesema inaratibu ujenzi wa kingo katika eneo hilo ili kukuabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

**************************

Na Lulu Mussa

Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa watekelezaji na wasimamizi wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (Ecosystem Based Adaptation for Rural Resilience – EBARR in Tanzania) unaotekelezwa Kaskazini A - Unguja kuongeza kasi ya uchimbaji wa visima katika eneo la Matembwe ili wakazi wa maeneo hayo waweze kunufaika na maji safi na salama.

Dkt. Jafo ametoa rai hiyo leo 28 Januari 2022 mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika eneo la Matembwe na kuzungumza na watendaji na wasimamizi wa mradi

huo na kuwaagiza kusimamia kazi zote zilizopangwa kutekelezwa na kuhakikisha zinakamilika kwa wakati bila kuomba muda wa nyongeza.

Amesema agenda ya mazingira ni suala linaloigusa dunia kwa sasa na kuainisha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na ni mjadala wa kidunia hivyo Ofisi yake itahakikisha inashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Zanzibar) katika kuibua miradi yenye manufaa kwa pande zote mbili za muungano.

“Ndugu zangu sote ni mashahidi wa athari hizi za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ukame na hapa Zanzibar visima viko hatarini kutoweka kutokana na ongezeko la kina cha bahari” Jafo alisisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Saada Mkuya ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza miradi ya maendeleo pande zote mbili za Muungano na kusisitiza kuwa atahakikisha shughuli zilizopangwa kutekelezwa na mradi huo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa boti, uchimbaji wa visima na utengenezaji wa majiko banifu unakamilika kwa muda uliopangwa bila kuomba muda wa ziada.

Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini ni wa kipindi cha miaka mitano na ulianza utekelezaji wake 2018 na unatekelezwa katika wilaya za Kishapu, Mvomero, Mpwapwa, na Simanjiro kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa Zanzibar mradi unatekelezwa katika Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja - Kijiji cha Matemwe, Mbuyutende na Matemwe Jugakuu.

Lengo la mradi huu ni kuongeza uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia na kuwezesha njia mbadala za kujiongezea kipato. Mradi huu unaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwa upande wa Zanzibar Mradi unatekelezwa kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira (Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais).

Jumla ya shilingi 1,100,112,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Mradi upande wa Kaskazini A, na kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuendesha mafunzo na kuviwezesha vikundi katika maeneo ya mradi kutengeneza majiko sanifu na banifu kwa lengo la kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa na hivyo kupunguza uharibifu wa misitu.

Pia, kuandaa Mipango ya Usimamizi wa Matumizi ya ardhi ili kuwezesha jamii husika kupanga matumizi ya ardhi kwa ajili ya Makazi, Kilimo, Ufugaji, Hifadhi ya Misitu/mikoko na uoto wa asili, hifadhi ya vyanzo vya maji ili kuepusha migogoro katika matumizi ya ardhi.

Kupitia mradi huu utafanyika ununuzi wa boti sita za uvuvi, Uchimbaji wa Visima Virefu sita (6) katika Shehia tatu za Kijini, Mbuyutende na Jugakuu na mpaka sasa jumla ya majiko sanifu 90 yametengenezwa katika kaya ya Matemwe Kijini, Matemwe Mbuyutende na Matemwe Jugakuu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments