HELVETAS TANZANIA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI UPANDAJI MITI


AFISA Mazingira Mkoa wa Simiyu Juma Kazula (mwenye tisheti ya kijani) akitoa elimu ya namna ya kuondoa kiriba kabla ya kupanda mti mbele ya wanafunzi wa sekondari Lubiga iliyopo wilayani Meatu mkoani humo, katikati ni Afisa Mazingira wilaya ya Meatu Thomas Shishwa.

***

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

Shirika lisilokuwa na Kiserikali la Helvetas Tanzania lenye makao makuu jijini Dodoma linatarajia kupanda miti zaidi ya elfu 16 mkoani Simiyu ili kuendelea kulinda Uoto wa Asili pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Shirika hilo ambalo pia linatekeleza miradi ya elimu, kilimo, vijana na utunzaji wa mazingira na kwamba miradi hiyi inatekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Rukwa, Katavi, Mbeya, Singida na Simiyu.

Aidha, Katika mikoa ya Simiyu na Singida ili kuwezesha akina mama kuweka akiba na kukopeshana ili kumudu hali ya uchumi na kujikwamua kimaisha pamoja shughuli za kilimo hai na utuzajia ili kurejesha uoto wa asili ikiwemo kupanda miti.

Afisa Mtathimini na Ufuatiliaji kutoka shirika hilo Loveness Msemwa anaeleza kuwa wanatekeleza miradi ya kuwezesha akina kuweka na kukopeshana, kilimo hai pamoja na utunzaji wa mazingira katika mikoa miwili nchini.

Anasema kupitia mradi wa kilimo hai unaotekelezwa mkoani Simiyu wanashirikiana na kampuni ya Alliance Ginnery na GIZ kutekeleza mradi wa kilimo hai ndani yake wakipanda miti ili kurejesha uoto wa asili kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kilimo hai kisichotumia mbolea wala kemikali za viwandani.

‘’Kilimo hai kinahitaji uoto wa asili, mazao yanayozalishwa hayahitaji mbolea za viwandani wala kemikali, hivyo sisi tunatunza mazingira kwa kupanda miti, wenzetu Alliance ginnery wanafundisha wakulima kilimo hai’’ anaeleza Loveness.

Anafafanua kuwa katika mkoa wa Simiyu, mradi huo unatekelezwa wilaya ya Meatu kwenye kata za Kisesa na Lubiga na wanatarajia kupanda miti 16,715 kwenye taasisi za umma na kila mwananchi atagawiwa miti mitano mitano bure.

‘’Lengo ni kuboresha mazingira katika taasisi za umma, kurejesha uoto wa asili na kufanya utunzaji wa mazingira endelevu…tumejikita kwenye taasisi za umma kwa sababu zina rasilimali watu wa kutunza miti hiyo’’ anasema Loveness.

Anafafanua kuwa kupitia kugawa miti mitano kila kaya, jumla ya kaya 2343 zatapanda miti na wataendelea kufuatilia ukuaji wa miti hiyo kwa sababu mradi huo unatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu.

Anasema kuwa wameshakutana na wananchi kupitia mikutano ya vijiji ili kuunda kamati za mazingira za vijiji na kwamba wajumbe wa kamati hizo wamekuwa mabalozi wazuri wa upandaji miti.

Anafafanua kuwa kamati hizo zimewasaidia kuzifikia taasisi za umma ikiwemo shule, zahanati, misikiti na makanisa na kwamba hadi sasa kila mwananchi anashiriki kupanda miti nyumbani kwake na kwenye taasisi.

Ofisa Mazingira wilaya ya Meatu Thomas Shishwa anawashukuru wadau wa maendeleo wanaojitokeza kupanda miti wilayani humo huku akiwataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kupanda miti katika maeneo yao.

Anasema lengo la Halmashuri ni kupanda miche milioni 1.5, kupitia kwenye taasisi za umma ikiwemo shule za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya pamoja na nyumba za ibaada lakini pia kila mwananchi atahakikisha anapanda miti mitano.

Hivi karibuni, Afisa Mazingira Mkoa wa Simiyu Juma Kazula alishiriki uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti iliyofanyika katika kata za Lubiga na Kisesa wilayani Meatu mkoani humo, na kuwataka wadau wa mazingira kujitokeza kuunga mkono juhudi za serikali kwenye upandaji miti.

Kupitia Mradi wa utunzaji mazingira unaotekelezwa na Helvetas Tanzania, Kazula anawataka wadau na wananchi kupandaji miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yanasababisha madhara makubwa kwa binadamu, wanyama na mimea.

Anayataja madhara hayo kuwa ni ukosefu wa mvua ambao husababisha ukosefu wa malisho, ukame, kukauka kwa vyanzo vya maji, kuongeza kwa joto, mmonyoko wa udongo na kuongezeka kwa hewa ukaa.

Kazula anataka jamii kutunza miti iliyopo pamoja na kuongeza kasi ya upandaji ili kuongeza uoto wa asili ambao unachangia kuleta mvua, kulinda vyanzo vya maji pamoja na kupunguza hewa ya kabondayoksaidi. 

Kazula anawashukuru wadau hao wa maendeleo kwa juhudi za kushirikiana na serikali kupanda miti ili kurudisha hifadhi ya mazingira ambayo ilikuwa imeanza kupotea kutokana na ongezeko la ukataji miti ovyo.

‘’Tunawashukuru Helvetas Tanzania kwa kushiriki kupanda miti wilaya ya Meatu ambao watatusaidia kufikia malengo ya upandaji miti…mpango wetu kila Halmashauri ni kupanda miti milioni 1.5 na kufanya mkoa mzima kuwa na jumla ya miti milioni 9 kwa mwaka mzima’’ Anasema Kazula.

Anasema wanaendelea kushirikiana na Wakala wa Misitu (TFS) pamoja na wazalishaji wengine wa miti ikiwemo kampuni ya Alliance ginnery ili kuifanya Simiyu kuwa ya kijani, huku akimtaka kila mwananchi kupanda miti mitano mitano katika eneo analoishi.

Anaongeza kuwa kupitia Helvetas Tanzania wamejikita zaidi kupanda miti kwenye taasisi za umma ikiwemo shule za msingi na sekondari, makanisani, misikitini pamoja na zahanati ili miti hiyo iweze kusimamiwa ipasavyo.

Oscar Kanuda mkazi wa Lubiga anawataka wananchi wenzake kushiriki kikamilifu upandaji miti katika maeneo yao ili waweze kurejesha uoto na asili hali ambayo tapungua majanga ya asili ikiwemo ukosefu wa mvua na ukame.

‘’Tunaishukuru serikali na wadau kwa kutuletea miti mpaka majumbani kwetu, niwaombe wananchi wenzangu tupande miti ili iweze kutusaidia baadae…miti inaleta mvua, inazuia upepo na pia inatunza vyanzo vya maji’’ anasema Kanuda.

Dotto Saimon Mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Lubiga aliwashukuru wadau wa mazingira kwa kuwaletea miti shuleni kwao ambapo alisema ikikua itazuia upepo, itatunza mazingira na vyanzo vya maji pia wataweza kupata kuni.

Naye Kabula Salehe mwanafunzi wa darasa la saba Lubiga shule ya msingi aliwataka wafunzi wenzake kuendelea kuitunza miti hiyo itakayowasaidia wanafunzi kupata hewa safi na kivuli wawapo shuleni.

Leticia Erasto mwanafunzi wa shule ya sekondari Lubiga anasema ameshiriki zoezi la upandaji miti shuleni hapo, huku akiwataka walimu kuwagawia wanafunzi kila mmoja miche ya miti ili aweze kuisimamia kuliko kuipanda kiholela.

‘’Tunawashukuru wadau walioleta miti shuleni, lakini niwashauri walimu wetu kila mwanafunzi agawiwe miti angalau miwili apande na kuisimamia hadi ikue ili tuweze kufika lengo la serikali pamoja na wadau la kupanda miti’’ anasema Mwanafunzi huyo.

Leticia anaiomba serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za upandaji miti ambapo baadhi ya maeneo yameathiriwa na ukosefu wa mvua, ukame na kuongezeka kwa joto ili jamii iweze kubadilika na kupanda miti ya kutosha.

Costantine Phabian, Afisa Kilimo kutoka Kampuni ya Alliance Ginnery anasema kampuni yao inajikita na kilimo hai ambacho hakitumii kemikali za viwandani na kinasaidia utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.

Anasema wanashirikiana na Helvetas kwenye mradi wa kilimo hai na ndani yake wanapanda miti katika kata za Kisesa na Lubiga ambapo Alliance wanahudumia wakulima kwenye vikundi vya kilimo hai wakiwa na lengo moja na kutunza mazingira.

‘’sisi sote ni wadau wa mazingira, lengo la kilimo hai ni kuhifadhi mazingira na kutunza uoto wa asili, kurutubisha ardhi na kulinda vyanzo vya maji pamoja na viumbe wengine…tunafundisha wakulima kuhifadhi ardhi na kutokata mito ovyo’’ anasema Phabian.

Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Masuala ya Jamii (ESRF) mwaka 2003 umebainisha kuwa mambo makuu yanayosababisha umaskini ni uchumi duni, uharibifu wa mazingira na kukosekana kwa utawala bora.

Sera ya Mazingira ya mwaka 1997 imeainisha matatizo makuu sita ya mazingira yanayoikabili nchi yetu, ambayo ni Uharibifu wa ardhi, Kutopatikana kwa maji safi kwa wakazi wa mjini na vijijini, Uchafuzi wa mazingira, Upotevu wa makazi ya viumbe pori na bioanuai, Uharibifu wa makazi ya viumbe wa majini na Uharibifu wa misitu.

Kutokana na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Taifa ya Hifadhi za Mazingira ya mwaka 2004 na Programu mbalimbali za kuhamasisha upandaji miti kila mwaka, ni dhahiri kuwa Serikali inahimiza wananchi na taasisi zishiriki kikamilifu katika suala la kupanda miti. 

Upandaji miti unaweza kufanywa na taasisi za serikali, makampuni ya wawekezaji, vikundi vya jamii, shule na hata watu binafsi na Watanzania wengi sasa hivi wanaelewa kuwa uchumi wa nchi na maisha yanategemea sana mazingira bora. 

Miti inaweza ikapandwa peke yake ikawa msitu, mti mmoja mmoja katika shamba, kuzunguka shamba, katika maeneo ya makazi, kando kando ya barabara na penginepo kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.

Mzee Oscar Kanuda (kushoto) akiwa na wanakiji wenzake wakishiriki zoezi la upandaji miti lililofanyika hivi karibuni shule ya msingi Lubiga, zoezi hilo liliratibiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Helvetas Tanzania.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Lubiga iliyopo wilaya ya Meatu mkoa Simiyu wakishiriki zoezi la upandaji miti lililokuwa likiendeshwa na shirika la Helvetas Tanzania hivi karibuni.
Wanafunzi wa shule ya msingi Lubiga iliyopo wilaya ya Meatu mkoa Simiyu wakishiriki zoezi la upandaji miti lililokuwa likiendeshwa na shirika la Helvetas Tanzania hivi karibuni.
AFISA Mazingira wilaya ya Meatu Thomas Shishwa (aliyechumaa) akikata kiriba kwa ajili ya kupanda miti shule ya msingi Lubiga iliyoko wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments