RAIS WA AFRIKA KUSINI AKUTWA NA COVID 19



Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amepimwa na kukutwa na Covid-19 na anatibiwa kwa dalili zisizo kali.

Bw Ramaphosa alianza kujisikia vibaya siku ya Jumapili baada ya kuondoka katika ibada ya kumbukumbu ya Rais wa mwisho wa enzi za ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini FW De Klerk mjini Cape Town, kulingana na taarifa kutoka kwa ofisi ya rais.

Watu ambao walitangamana na rais siku hiyo wameshauriwa kutazama dalili au kupimwa.

Rais amepewa chanjo kamili na amekabidhi majukumu yake yote kwa Naibu Rais David Mabuza.

Rais Ramaphosa alirejea Jumatano iliyopita kutoka katika ziara ya nchi za Afrika Magharibi za Nigeria, Ivory Coast, Ghana na Senegal.

Rais alisema yeye na ujumbe wake walipimwa Covid katika nchi zote walizotembelea. Taarifa hiyo ilisema rais alikuwa amepatikana bila virusi hivyo aliporejea.

Kirusi cha Omicron kinachoambukiza sana, ambacho kimezua wasiwasi wa kimataifa, kilitambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini mwezi uliopita.

Chanzo - BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments