SERIKALI YATENGA BILIONI 10.5 KWA AJILI YA UJENZI WA VITUO VYA MICHEZO DAR, DODOMA NA GEITA


Naibu Waziri,Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Paulin Gakul akiongea na Vyombo vya habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwenye Wizara hiyo tangu Uhuru.
Naibu Waziri,Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Paulin Gakul akiongea na Vyombo vya habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwenye Wizara hiyo tangu Uhuru.
***
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog,Dodoma.

SERIKALI kupitia Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo, imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya michezo katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita na Dodoma huku akisisitiza kuwa hatua hiyo ni moja ya mafanikio makubwa ambayo  imeyapata katika kipindi cha miaka 60.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo Pauline Gekul ameeleza hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo tangu kipindi cha uhuru ikiwa ni mwendelezo wa mfululizo wa hotuba za wakuu wa Wizara ulioandaliwa na Idara ya habari-Maelezo kwa lengo la kuhabarisha umma mwelekeo,mafanikio na mahali ilipo Tanzania tangu kupatikana kwa uhuru.

Amesema kwa upande wa miundombinu ya Michezo, Tanzania imepiga hatua kubwa ambapo viwanja vya michezo mbalimbali vimeboreshwa na kujengwa na Serikali pamoja na wadau wa Michezo.

Amevitaja viwanja hivyo ni pamoja na Uwanja wa Benjamini Mkapa uliogharimu Sh Bilioni 56.4, Kituo cha Michezo cha JK Park, Majaliwa Stadium – Ruangwa, Azam Complex, Black Rhino – Karatu, Ngarenaro Complex, Kilimanjaro Golf Club, na Lugalo Golf Club kwa uchache.

“Viwanja vya Uhuru, Nyamagana na Kaitaba kuwekewa nyasi bandia, kuboreshwa kwa uwanja wa Ndani wa Taifa pamoja na kuwekwa taa kwa viwanja vya Jamhuri Dodoma na Majaliwa Stadium katika mwaka wa fedha wa wa 2021.

Naibu Waziri huyo ameeleza pia Serikali kupitia Wizara hiyo bado haijaachana na mchakato wa kupata vazi la Taifa na kuwataka watanzania  kuendelea kubuni vazi hilo .

Kuhusu mafanikio kwa Sekta ya Utamaduni, Gekul amesema tangu  kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika kwa sasa Tanzania Bara, kumeshuhudia mafanikio mbalimbali katika Sekta ya Utamaduni nchini ikiwemo kukua kwa fani mbalimbali za Utamaduni zikiwemo Sanaa, Malikale, Makumbusho na Nyaraka.

“Kukua kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Mwaka 2006 Kiswahili kilipitishwa rasmi kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Afrika; mwaka 2019 Kiswahili pia imekuwa lugha rasmi katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),”amesema.

SANAA.  

Gekul amesema tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika kwa sasa Tanzania Bara, kumeshuhudia mafanikio mbalimbali katika Sekta ya Sanaa nchini ambayo ni pamoja na  kuanzishwa kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo mwaka 1984 Serikali ilitunga Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa namba 23 ambayo ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

“Pamoja na majukumu mengine husajili wasanii, kutoa vibali vya shughuli za sanaa, kuwatetea wasajiliwa wake, kuwatafutia masoko ya kazi zao na kusimamia uanzishwaji wa mashirikisho ya sanaa nchini. Kuwepo kwa Baraza kumeifanya sekta ya sanaa kushamiri hadi kufikia sekta hiyo kuongoza katika ukuaji wa pato la taifa kwa mwaka 2018/2019 kwa asilimia 13.7,”amesema.

Amefàfanua kuwa  kipindi hiki, kumeanzishwa Taasisi ya Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) ambapo mwaka 1976 Serikali ilianzisha na kuitambua kama Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania. TFB ilianzishwa kwa Sheria Namba 4 ambayo husimamia masuala yote ya filamu na michezo ya kuigiza.

"Wizara inajivunia kuanzishwa kwa mifumo ya kielektroniki ya kusajili wasanii, kutoa vibali na leseni, pamoja na kufuatilia kazi za wasanii kwenye vyombo vya habari na mitandaoni ambapo Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA, Bodi ya Filamu Tanzania – BFT na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania – COSOTA wamekamilisha mifumo ya kielektroniki,"amesema

MICHEZO 

Naibu Waziri huyo amesema  Tanzania imefanikiwa kupata jumla ya Medali 16 katika michezo mikubwa  duniani katika michezo ya   Olympic (2); Jumuiya ya Madola (7); na Michezo ya Bara la Afrika (7); na kwamba timu zetu zimeshiriki katika michezo  mikubwa bila kukosa tangu Nchi ipate uhuru.

Amesema Tanzania imefanikiwa kuwa na wachezaji wakulipwa katika nchi mbalimbali tangu Uhuru na kwamba hadi sasa ina jumla ya wachezaji 54 wakulipwa katika nchi mbalimbali ambapo (28) ni wachezaji wa mpira wa miguu, (16) mpira wa kikapu, (4) mpira wa wavu, (2) Kabbadi, (2) Netiboli (1) kuogelea na (1) mchezo wa Roliball;

"Tuko vizuri kimichezo,Tanzania imeshinda vikombe mbalimbali katika mashindano ya kimataifa tangu kupata uhuru wake ambapo kwa upande wa mpira wa miguu kwa wanawake, Tanzania imechukua vikombe vitano (5) katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,"amefafanua Gekul.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments