Picha : RAIS SAMIA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KUKAGUA UJENZI WA DARAJA LA TANZANITE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 04 Novemba, 2021 amerejea Jijini Dar es Salaam akitokea Glasgow, Scotland alipokuwa akihudhuria Mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26).

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Aidha, Mhe. Rais Samia amefanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Tanzanite linalojengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amepokea maelezo ya ujenzi wa daraja hilo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Mhandisi Rogatius Mativilla ambaye amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 98.44.

Mhandisi Mativila amesema daraja hilo litakapokamilika litapunguza msongamano wa magari, ajali bararani, litaboresha hali ya maisha Jijini Dar es Salaam pamoja na kupendezesha jiji la Dar es Salaam na kuwa sehemu moja wapo ya kivutio cha utalii katika fukwe zilizopo karibu na daraja hilo.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amefanya ziara katika eneo la Coco Beach ili kuona agizo lake la kutaka wafanyabiashara wadogowadogo kupangwa vizuri katika mazingira bora ya kufanya biashara linavyoendelea kutekelezwa.

Aidha, Mhe. Rais amesema ziara hiyo pia imemuwezesha kuona hali halisi ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Coco beach na kusema kuwa Serikali itaangalia upya namna ya kuzuia athari hizo.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali itaendelea kuwajali wafanyabiashara wadogo wadogo na kutolea mfano eneo hilo ambalo wafanyabiashara wakubwa walilitaka lakini Serikali ilikataa kwa kujali maslahi ya wafanyabiashara wadogo ili waendelee kukuwa na kujipatia kipato.

Pia, Mhe. Rais amesema Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo ambao itabidi kuzirejesha ili kuwezesha wengine kupata mikopo hiyo na kuendeleza biashara zao.

Mhe. Rais Samia amesema zoezi la lengo la kuwapanga wafanyabiashara wadogo wadogo mijini ni zuri ambalo limelenga kuwaboreshea mazingira yao ya biashara, kuweka miji katika hali ya usafi pamoja na kuimarisha usalama.

Vilevile Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango Pamoja na TAMISEMI kuanza mara moja ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo kwasababu tayari Serikali imepata fedha kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 34 ambapo ujenzi huo utahusisha soko la zamani na kujenga mengine mawili mapya ya kisasa mkabala na soko la zamani la Kariakoo na kujenga soko jingine jipya katika eneo la Jangwani Jijini Dar es Salaam.

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Tanzanite linaloendelea kujengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021. Kulia ni mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatius Mativila.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatius Mativila kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Tanzanite linaloendelea kujengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na wafanyabiashara wadogowadogo katika eneo la Coco Beach Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na wafanyabiashara wadogowadogo katika eneo la Coco Beach Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kushtukiza leo tarehe 04 Novemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohammed Gharib Bilal alipomtembelea kumjulia hali nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam leo tarehe 04 Novemba 2021.


Ujenzi wa Daraja jipya la Tanzanite (Tanzanite) lenye urefu wa mita 1030 limefikia asilimia 98.44 na linatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba 2021. 
Mandhari ya eneo la fukwe la Coco Beach ambapo wafanyabiashara wamejengewa Vibanda vya biashara. PICHA NA IKULU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments