SINDANO YA KUDHIBITI VIRUSI VYA UKIMWI KWA MUDA MREFU ZAIDI YAIDHINISHWA UINGEREZA





Maelfu ya watu wanaoishi na virusi vya HIV sasa watakuwa wanapewa sindano mpya yenye ufanisi wa muda mrefu ili kudhibiti hali zao iwapo watataka kuacha kumeza vidonge kila siku.

Mashirika ya misaada yameafiki idhini hii ya matibabu ya taasisi ya usimamizi wa madawa nchini Uingereza NHS nchini Uingereza.

Sindano hii husitisha makali ya virusi, sawa na dawa za kawaida za antiretroviral .

Inakadiriwa kuwa watu 13,000 nchini Uingereza wanaweza kuamua kudungwa sindano hiyo badala ya vidonge.

Dawa hiyo ya sindano inayofahamika kama Cabotegravir (pia ikiitwa Vocabria na kutengenezwa na ViiV Healthcare) na rilpivirine (pia ikiitwa Rekambys na kutengenezwa na Janssen) hutolewa kama sindano mbili tofauti kila baada ya miezi miwili.

Tiba hiyo ni bora tu kwa wale ambao wameweza kufanikiwa kufikia viwango vya kutogundulika kwa virusi katika damu yao wakati wanapomeza vidonge.

Wataalamu wanasema tiba hii ya sindano inaweza kuwa rahisi kutumiwa na wengi.

Profesa Chloe Orkin, ambaye ni mtaalam wa HIV katika Chuo kikuu cha Queen Mary cha London, amesema itawapunguzia mzigo watu wenye HIV ambao wamekuwa wakilazimika kumeza vidonge kila siku na badala yake kuwapatia tiba mara sita tu kwa mwaka.

Dokta Sanjay Bhagani, rais taasisi ya tiba ya Ukimwi - European Aids Clinical Society, amesema "Hili limepokelewa vyema kabisa.

"Bado unyanyapaa umesalia kuwa suala kuu katika jamii ya watu wenye HIV, na kumeza tembe kila siku ni jambo linaloweza kuwa gumu miongoni mwa baadhi ya watu. Hii inatoa tiba mbadala ya sindano kwa wengi.


"Data na tafiti zinazoshauri tiba hii ni imara, na uzoefu halisi wa dunia unaonyesha kwamba wagonjwa wanaoanza kwa tiba za sindano hupendelea kuendelea nazo ."



Alex Sparrowhawk, kutoka Manchester, anafanya kazi katika shirika la msaada linalowasaidia wanaoishi na HIV linaloitwa Terrence Higgins Trust.


Alipatikana na HIV miaka 12 iliyopita na amekuwa akipokea dawa za ART tangu wakati huo. Anasema kuwa na chaguo tofauti la tiba ni jambo la kufurahisha.


"Habari mpya ni kitu ambacho watu wengi wamekuwa wakikisubiri.


" Wazo la kudungwa sindano mara sita kwa mwakabadala ya kumeza vidonge kila siku bila shaka linafurahisha. Kukumbuka kumeza vidonge kila siku ni ukumbusho wa kila siku wa HIV na kuiweka mbele na kati kati. Huwezi kuiepuka wala kuisahau.


"Watu wengine wanaweza kuishi na watu ambao hawafahamu hali zao za HIV au wafanye kazi kwa zamu katika kiwanda ambazo zinawepeleka katika maeneo mbali mbali ya dunia, na kuwa changamoto ya kupata matibabu ya kila siku ."


Anaamini wale wanaohitaji zaidi tiba mpya, kama vile wake wanaonyanyapaliwa zaidi, wanafaa kupewa kipaumbele kupewa tiba ya sindano.

Chanzo - BBC Swahili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments