WAZIRI MKUU AMUWAKILISHA RAIS SAMIA KATIKA MAZISHI YA OLE NASHA

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge Ngorongoro na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, William Tate Ole Nasha na amewasihi wananchi wamuenzi kwa kuyaendeleza mambo mazuri yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye ameshiriki katika mazishi hayo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha Ole Nasha ni pigo kubwa kwa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bunge pamoja na kwa wanafamilia na wananchi wa Ngorongoro.

Mazishi hayo ya Ole Nasha yamefanyika leo (Jumamosi, Oktoba 2, 2021) nyumbani kwake katika kijiji cha Osinoni kata ya Kakesyo wilayani Ngorongoro mkoa wa Arusha. Mbunge huyo alifariki Jumatatu, Septemba 27, 2021 mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia anawataka Watanzania waenzi mambo mazuri yote aliyoyafanya marehemu Ole Nasha ili jamii aliyokuwa anaiongoza inufaike. “Marehemu amefanya mambo mengi na ametoa mchango wa hali ya juu kwa Serikali.”

Amesema jambo la muhimu kwa sasa ni kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema. “Mke wa marehemu, watoto, ndugu, jamaa na wabunge nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.”

Kwa upande wake, Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu –Uwekezaji, Geofrey Mwambe amesema Serikali hususani Ofisi ya Waziri Mkuu imepata pigo kubwa kwa kumpoteza mpiganaji kwa sababu marehemu Ole Nasha alikuwa mtumishi hodari.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Dkt. Martin Ngoga, viongozi wa Serikali, wabunge pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.


(Mwisho)
IMETOLEWA NA



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments