GUGU KONGWA LATISHIA USTAWI WA MALISHO YA MIFUGO KANDA YA KATI

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah (wa pili kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika jijini Dodoma jana.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Antony Sangeda akiwasilisha sehemu ya utafiti wa Gugu Kongwa kwa Wadau wa Sekta ya Mifugo katika Mkutano wa uwasilishaji wa Utafiti huo uliofanyika jijini Dodoma jana.
Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Prof. Erick Komba akitoa maoni yake  katika Mkutano wa uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika jijini Dodoma jana.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri  Gillah (kulia) akiwa na wadau wengine wakifuatilia uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika  jijini Dodoma jana.



Na Mbaraka Kambona,


WATAFITI kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na Serikali wamesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka za kudhibiti kusambaa kwa mmea wa Gugu Kongwa ambao umeonesha kuathiri kwa kiasi kikubwa maeneo ya malisho  yaliyopo wilayani Kongwa na mkoani Singida.

Hayo yalibainishwa na Wataalamu hao walipokutana na wadau wengine wa Sekta ya mifugo jijini Dodoma Oktoba 22, 2021 kuwasilisha  matokeo ya awali ya utafiti waliofanya kujua tabia za ukuaji na usambaaji wa mmea huo ili kutafuta njia fungamanishi za kupunguza au kutokomeza kabisa mmea huo ujulikanao Gugu Kongwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mtafiti Kiongozi kutoka SUA, Dkt. Selemani Ismail alisema utafiti wa Gugu Kongwa ulilenga kujua tabia ya ukuaji wake na  kwa kiasi gani mmea huo unaoathiri malisho ya Mifugo umesambaa.

"Utafiti wa awali tulioufanya kwa miaka miwili (2)  ulilenga kutafuta njia shirikishi za kupunguza au kuangamiza kabisa mmea huo wa Gugu Kongwa ambao usambaaji wake umekuawa na athari kubwa katika maeneo mengi ya malisho hususan katika maeneo ya Kanda ya Kati na Mkoa wa Manyara," alisema Dkt. Ismail

Dkt. Ismail aliendelea kusema kuwa katika kutafuta njia ya kudhibiti Gugu Kongwa walifanya utafiti na kupata mmea unaoitwa Melia ambao umeonesha ufanisi katika kutokomeza usambaaji wa Gugu Kongwa.

"Utafiti wetu tuliufanya Wilayani Kongwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ili kutokomeza mmea huo na kulinda malisho kwani likiachwa liendelee kusambaa athari zake ni kubwa sana kwa malisho ya mifugo," aliongeza

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inajipanga kuhakikisha matokeo hayo ya utafiti yanakwenda kufanyiwa kazi.

"Tumeona athari kubwa za gugu hili vamizi katika maeneo yetu ya malisho na hivyo ni muhimu kulidhibiti mapema ili lisisababishe uhaba wa malisho na kupunguza tija katika uzalishaji," alisema Dkt. Gillah

Meneja wa Mfuko wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Ntufye Mwakigonja alisema anaimani kuwa utafiti huo utatatua changamoto hiyo inayokabili malisho nchini huku akiongeza kuwa  wao kama COSTECH wataendelea kushirikiana na watafiti hao ili kuhakikisha matokeo hayo yanafanyiwa kazi kwa manufaa ya sekta ya mifugo nchini.

Aidha, Wadau wa Sekta ya Mifugo waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa pamoja na kuwepo  changamoto zinazosababishwa na mmea huo katika malisho ya mifugo, watafiti hao waendelee kufanya utafiti kuangalia mtizamo chanya ambao unaweza kusaidia jamii kutumia faida zinazoweza kupatikana zitokanazo na Gugu Kongwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments