Wajumbe Wa Kongamano La Misri Wakubaliana Kukuza Uchumi Licha Ya Covid 19

 Na. Josephine Majula, WFM – Cairo Misri
Wajumbe wa Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri (Egypt International Cooperation Forum) ikiwemo Tanzania wamekubaliana kutoa ripoti ya tathimini ya mkutano huo baada ya miezi mitatu ambapo yote yaliyojadiliwa na kukubaliwa likiwemo suala la kuendeleza ukuaji wa uchumi licha ya changamoto ya Covid 19 yatatolewa mwongozo kwa ajili ya utekelezaji.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba wakati wa kuhitimisha Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri (Egypt International Cooperation Forum) lililofanyika kwa siku mbili mjini Cairo nchini Misri.

Dkt. Mwigulu alisema kongamano hilo limemalizika na ajenda mbalimbali zilijadiliwa zikiwemo za mikakati ya kupambana na Uviko- 19 na umuhimu wa mahusiano ya kimataifa katika kujijenga kiuchumi.

Katika hatua nyingine Dkt. Mwigulu alitembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Misri ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Misri Mhe. Meja Jenerali Anselm Bahati.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Daniel Sillo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban na wataalamu kutoka wizara hiyo.

MWISHO.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments