SERIKALI YAKAMILISHA MWONGOZO WA KITAIFA KUWEZESHA WAHITIMU WA KADA ZA AFYA KUAJIRIWA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Wednesday, September 15, 2021

SERIKALI YAKAMILISHA MWONGOZO WA KITAIFA KUWEZESHA WAHITIMU WA KADA ZA AFYA KUAJIRIWA

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini imekamilisha mwongozo wa kitaifa wa kuwawezesha wahitimu wa kada za afya ambao hawana ajira rasmi, waweze kuajiriwa kwa muda.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri Jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wamekamilisha mwongozo wa Kitaifa wa Kujitolea (National Health Workforce Volunteerism Guideline) unaotoa utaratibu wa namna bora ya Hospitali na Vituo vya afya kutumia wahitimu wa kada ya afya ambao hawajaajiriwa ili waweze kutumika rasmi katika utoaji wa huduma za afya kwa njia ya kujitolea.

“Mwongozo huo ni mkakati mahususi wa kuboresha huduma za afya kwa kukabiliana na uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya nchini hii hapa ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa upatikanaji na utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi”, amesema Waziri Gwajima.

Waziri Gwajima, amesema, Serikali ya awamu ya sita inaendelea kutekeleza Afua za Sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 2,726 wa kada za Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, lengo likiwa ni kuikamilisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima amesema Mkutano huo ambao umebebwa na kaulimbiu isemayo Ustahimilivu wa Mifumo ya Afya katika Mapambano dhidi ya UVIKO-19; ‘changamoto na fursa’ unatoa ishara ni kwa namna gani wataalam wa afya wanavyoshirikiana kutekeleza majukumu yao wanapo kabiliana na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (UVIKO -19) tokea ulipoingia hapa nchini.

“Pamoja na changamoto zilizopo, mmeendelea kujitoa na kutumia weledi wenu katika kuihudumia jamii, hili ni jambo la kizalendo, hongereni sana, nichukue nafasi hii kuwaelekeza viongozi wote wa ngazi zote kushiriki kuwahamasisha wananchi kwenda kupata chanjo ya UVIKO -19 kwani chanjo hizo ni Salama", amesisitiza Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, amesema serikali kuanzia awamu ya tano na ya sita zimekuwa zikitoa kipaumbele katika huduma  za fya, ambapo katika mwaka fedha wa 2021/22, jumla ya Hospitali 28 zinakwenda kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya ambazo hazikuwepo kabisa, aidha Tarafa zote 207 zitajengewa Vituo vya afya huku Tarafa 150 zikiwa tayari zimeshapelekewa fedha katika mwanzo wa mwaka kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Dkt. Dugange Amewakumbusha Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri, kusimamia ipasavyo rasilimali zote zinazofika kwenye maeneo yao huku akiwataka kutumia Mkutano huo kama sehemu ya darasa la kujifunza katika kukabiliana na Uviko-19  kwa kubadilisha uzoefu kutokana na changamoto kutofautiana.

Akitoa salaam za Wizara ya Afya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi, amehimiza suala la uimarishaji wa utoaji wa huduma kwani Pamoja na kujenga miundombinu lakini saula la msingi ni uimarishaji wa utoaji huduma za afya, amesema watoa huduma lazima wawe na lugha zisizo za kumkera mtu anayepatiwa huduma.

Naye Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, yeye amewataka Waganga wakuu wa Mikoa kuwa mstari wa mbele katika suala la kuchanja, aidha Wizara itafatilia kujua Mkoa na Halmashauri kinara katika zoezi la kuchanja chanjo ya Uviko-19.

Mapema akiongea  katika Mkutano huo, Dkt. Florence Temu, kutoka AMREF na mwakilisi wa Non state Actors, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudu kubwa zinazo chukuliwa katika mapambano dhidi ya Uviko-19, na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali.

“Awali kulikuwa na vituo vya kutolea huduma za chanjo 500 lakini kwa takwimu za sasa  inaonesha idadi ya vituo hivyo imeongezeka na kufikia 1500, hii ni hatua kubwa, tunaimani Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau lakini pia kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za Uviko-19", amesema Dkt. Florence.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages