DADA AUAWA KWA KUKATWA PANGA AKITUHUMIWA KUMROGA BABA MKWE WAKE KAHAMA


Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwanamke aitwaye Limi Kulwa (30) ameuawa kwa kukatwa na panga sehemu za kichwani, usoni, na mikono yote miwili katika kijiji cha Ilunga, kata ya Iyenze, Manispaa ya Kahama mkoa wa Shinyanga akituhumiwa kumuua kwa kumroga baba mkwe wake aitwaye Lusana Kulwa (60).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio hilo limetokea Septemba 27,2021 majira ya saa mbili na nusu usiku katika kijiji cha Ilunga, kata ya Iyenze, Manispaa ya Kahama.

“Limi Kulwa mwenye umri wa miaka 30 wa ilunga aliuwawa kwa kukatwa na panga sehemu za kichwani, usoni, na mikono yote miwili na mwanaume mwenye miaka umri wa miaka 24 na mkazi wa kijiji cha Ilunga”,amesema

“Mtuhumiwa hajakamatwa, alitoroka baada ya kufanya mauaji. Mbinu iliyotumika ni kumvizia marehemu wakati anapika chakula nje ya jiko lake na kumkata kwa kutumia panga. Eneo la tukio kumekutwa panga moja lenye damu”,ameeleza Kamanda Kyando.

Amesema kiini cha tukio hilo ni imani za kishirikina ambapo marehemu alikuwa akituhumiwa kumuua kwa kumroga baba mkwe wake aitwaye, Lusana Kulwa (60) mkazi wa kijiji cha Ilunga ambaye alifariki kwa maradhi mwezi Julai,2021.

Amesema watuhumiwa sita wa familia hiyo wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na upelelezi ukikamikika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

“Napenda kutoa rai wananchi kujiepusha na vitendo hivi kwani siku zote uhalifu haulipi. tujiepushe na imani hizi za ushirikina ni imani potofu na hazina uhalisia wowote”,amesema Kamanda Kyando.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments