BOT KUTOA LESENI BIASHARA YA FEDHA ZA KIGENI

 Na.  Rahma Taratibu, Sandra Charles na Regina Frank, SJMC, Dodoma.
Serikali imeelekeza maduka yaliyofungwa pamoja na makampuni yanayotaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini kuomba leseni Benki Kuu ya Tanzania kwa kuzingatia matakwa ya sheria za fedha za kigeni.



Hayo yalielezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo aliyeuliza hatma ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha nchini (Bureau de Change) yaliyofungwa na Serikali nchini kote.

“Hadi kufikia tarehe 30 Julai 2021, Benki Kuu ilikua imepokea maombi mapya manne ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo yanafanyiwa uchambuzi na wahusika watapewa leseni iwapo watakuwa wamekidhi vigezo,” alisema Mhandisi Masauni.

Alifafanua kuwa ukaguzi uliofanyika mwaka 2018/19 ulipelekea maduka mengi ya kubadilisha fedha za kigeni kufungwa kutokana na kubainika kuendesha biashara bila kuzingatia sheria na kanuni husika.

“Baada ya kufungwa kwa maduka hayo, benki za biashara nchini zilihamasishwa kuendelea kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni katika matawi yake yote nchini na sasa benki zote za biashara zinatoa huduma hizo kote nchini,” alisema Mhandisi Masauni.

Aidha, Mhandisi Masauni alisema maduka ambayo hayakufungwa yameendelea kufungua matawi na kutoa huduma hizo katika miji mbalimbali nchini na kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ni ya kuridhisha.

Kwa upande wake Mbunge wa Mufindi Kusini Mhe. David Mwakaposa Kihenzile, aliuliza mkakati wa Serikali wa kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo ili sekta ya michezo iweze kustawi.

Akijibu swali hilo Mhandisi Masauni alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali imetoa msahama wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyasi bandia kwa viwanja vya mpira vilivyopo kwenye manispaa na majiji.

“Serikali itaendelea kutoa msamaha wa VAT kwenye nyasi bandia kwa viwanja vya mpira vilivyopo kwenye halmashauri baada ya kuridhishwa na matumizi ya msamaha uliotolewa kwenye manispaa na majiji, ”alisema Mhandisi Masauni.

Aliongeza kuwa katika kuendeleza Sekta ya michezo Serikali imetoa msamaha wa VAT kwenye huduma za elimu zitolewazo kwenye vituo vya mafunzo ya michezo.

MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments