MTU MMOJA AFARIKI, WENGINE 8 HOI KWA KULA NYAMA YA KUKU MGONJWA
Binti mwenye umri wa 7 kutoka kijiji cha Igumo wadi ya Marimanti katika Kaunti ya Tharaka Nithi nchini Kenya ameaga dunia, huku watoto wengine saba na mtu mzima mmoja wakilazwa hospitalini baada ya kula kitoweo cha kuku aliyekuwa mgonjwa.

Charity Kaindi aliiambia Citizen Digital kwamba mwanawe aliitwa na babu yake Jumatatu jioni na kupelekwa nyumbani kwake, ambapo walishiriki mlo wa kitoweo cha kuku kabla ya kurejeshwa kwao jioni. 

Muda mfupi baadaye, alisikia mvurugano katika boma la jirani yake ambaye pia ni jamaa wake, alipokimbia huko kuona kilichokuwa kikiendelea alibaini kuwa mtoto mwingine alikuwa pia amekula kitoweo hicho na alikuwa anaumia tumbo.

Watoto wengine pia walianza kulalamikia maumivu ya tumbo na hapo akalazimika kumpigia simu mumewe ambaye anafanya kazi katika soko la Marimanti ili watoto walioathiriwa wakimbizwe hospitalini.

Baada ya hali yao kuwa mbovu, ilibainikwa kuwa jumla ya watoto wanane walikuwa wamekila kitoweo cha nyama ya kuku huyo kutoka boma la babu yao kwa jina Karong’o Makembo.

 Mmoja wa watoto hao Freida Nyambura aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya Marimanti Level 4 alisema kuwa babu yake alimletea nyama hiyo mahali pake pa kazi lakini alishindwa kuimaliza kwa sababu ilikuwa na harufu mbovu.

 Alidokeza kwamba muda mfupi baadaye alianza kuumwa na tumbo, kuhisi kisunzi, kuona giza na kutokwa na povu mdomoni.

 Alikimbizwa katika hospitali mara moja. Kwa bahati mbaya mmoja wa watoto kwa jina Linet ambaye alikuwa mahututi alifariki dunia akipokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Chuka akiwa ICU.

 Mmoja wa wanawe Karongo alithibitisha kuwa kuku huyo alikuwa mgonjwa alipochinjwa ila alidokeza kwamba tukio kama hilo halijawahi shuhudiwa licha yao kuwala kuku wanaougua.

Daktari Mwangangi ambaye anahudumu katika hospitali ya Marimanti Level 4 alithibitisha kisa hicho amacho alisema kilitokana na chakula chenye sumu.

 Alifichua kuwa matapishi ya waathiriwa yalikuwa na harufu kali. Waathiriwa wengine wanaendelea kupata nafuu hospitalini.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post