SERIKALI YAAGIZA MAOFISA MAENDELEO YA JAMII, USTAWI WA JAMII KUHAMASISHA WAZEE WAPATE CHANJO YA UVIKO - 19


Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mwanaidi Ali Khamis

Na Dotto Kwilasa, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya  Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto imewataka  Maafisa  ustawi na maofisa Maendeleo ya jamii  kuwahamasisha wazee wote nchini kujitokeza kupata chanjo ya UVICO-19 kwa hiari yao katika vituo vinavyotoa   chanjo hiyo.

Akiongea jana Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mwanaidi Ali Khamis amesema kundi la Wazee ni  miongoni mwa makundi yaliyopewa kipaumbele katika kutekeleza mpango huo wa kinga hivyo  watoa huduma za afya wanapaswa kuwapa kipaumbele.

"Wazee ni kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UVIKO 19 nawasisitiza mtilie mkazo jambo hilo kwa sababu wazee ni tunu ya Taifa ambao wanastahili kulindwa na majanga mbalimbali ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama wa afya zao,"amesema na kuongeza;

“Kwa kuwa uzee na kuzeeka unaambatana na upungufu wa kinga ya mwili, Serikali inatoa wito kwa wazee wote nchini kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya chanjo ya UVIKO 19 inayotolewa bure katika vituo mbalimbali vilivyoainishwa”,amesema.

Pamoja na mambo mengine  Naibu Waziri huyo aliiasa jamii kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi na tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.

"Tukifuata miongozo yote ya kijikinga na Corona tutafanikiwa na kuendelea na shughuli zetu za uzalishaji Kama waida bila kuwa na hofu ,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments