PROF : CHAGGU: MATUMIZI YA MAKAA YA MAWE HUPUNGUZA UKATAJI MITI OVYO


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Prof. Esnat Chaggu (aliyesimama), akitoa salamu ya utambulisho kwa uongozi wa Mgodi wa Tancoal baada ya kuwasili katika Mgodi huo.
Mtaalam wa Miamba Bwa. Matiko Paul akitoa ufafanuzi kwa Bodi ya Wakurugenzi wa NEMC juu ya namna wanavyofanya shughuli zao katika Mgodi wa Ngaka.

Mkurugwnzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka (aliyenyanyua mkono), akizungumza jambo kwa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC wakati walipokuwa wakikagua Mgodi.
Sehemu ya Miamba inayotumika kutolea makaa ya mawe katika Mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.

********************

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Prof. Esnat Chaggu amesema kuwa, matumizi ya makaa ya mawe ni nishati mbadala ambayo inasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuni hivyo kupelekea kupungua kwa kiasi kikubwa cha ukataji miti.

Ameyasema hayo alipokuwa katika Mgodi wa makaa ya mawe ya Ngaka uliopo kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, unaomilikiwa na Kampuni ya Tancoal Energy Limited, amesema kuwa makaa ya mawe ni muhimu sana kwa ajili ya nishati mbadala kama inavyofahamika kilele cha maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani mwaka huu Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesisitiza kutumia nishati Mbadala kuepuka ukataji miti hovyo.

Aidha Prof Chaggu ameeleza kuwa makaa ya mawe yanaweza kutumika katika Taasisi mbalimbali ikiwemo shule, jeshi na hata majumbani kama nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC Prof. Hussein Sosovere amesema kuwa, Bodi imetembelea mradi huu kuona shughuli za uchimbaji wa madini kama zinazingatia matakwa ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004. Amesema kuwa mradi huu unafaida lakini kunachangamoto nyingi za kimazingira kama haujazingatiwa ipasavyo, changamoto hizo ikiwemo uchafuzi katika vyanzo vya maji, kelele na vumbi.

“Hivyo tunawahimiza kampuni hii na NEMC kwa pamoja kushirikiana katika kuhakikisha vyanzo vya maji havichafuliwi, ili kuweza kuepusha uchafuzi wa mazingira na afya za binadamu kuwa salama” Prof Sosovere

Naye Meneja wa NEMC Kanda ya Kusini Bwa.Jamal Baruti amesema kuwa, kila shughuli inayofanywa na binadamu inaathari kwa mazingira, hivyo ni jukumu la Baraza na jamii kuhakikisha uwekezaji wowote unafanyika bila ya kuathiri mazingira.

“Sisi kama Baraza ikiwa kama jicho katika kusimamia mazingira, tumeweza kutoa ushauri na maelekezo katika suala la udhibiti wa vumbi na maji machafu ya mgodi ambayo yanaweza kusababisha uchafuzi katika vyanzo vya maji. Hivyo nitoe wito kwa makampuni mengine yanayohusika na uchimbaji wa makaa ya mawe wahakikishe wanatekeleza maelekezo yote waliyoelekezwa ili kulinda mazingira.” Bwana Baruti

kwa upande wake Meneja wa Mazingira na Usalama wa Tancoal Bwa. Fericks Bida amesema Kampuni inazingatia maelekezo wanayopewa na Baraza kwa kuhakikisha ulipuaji wa miamba unakuwa katika viwango vinavyokubalika isizidi mitetemo itakayoleta madhara kwa watu waliokaribu na mgodi. Kwa upande wa maji yanayotoka kwenye mgodi wanahifadhi katika mabwawa yaliyochimbwa kwenye mgodi ili kuepusha yasisambae na kwenda kwenye vyanzo vya maji.

Vile vile Bodi ya NEMC imetembelea Mto Luhuhu unaotenganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe, katika ziara hiyo Bodi imebaini uchafuzi mkubwa wa mto huo na kupelekea mto kujaa udongo na kina cha mto kupungua pamoja na maji ya mto kubadilika rangi kuwa mekundu. Bodi ya Wakurugenzi ya NEMC ipo kwenye ziara katika Kanda ya Kusini kukagua utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments