KALEMANI ASHUSHA UMEME TOKA 3700/- MPAKA 100/- KWA UNIT VISIWANI - MWANZA


Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani Julai 18, 2021 amefanya Ziara katika kisiwa cha Maisome kilichopo wilaya ya Sengerema jijini Mwanza na kuagiza kampuni binafsi ya Jumeme inayosambaza Umeme katika kisiwa hicho kutoza bei elekezi na Serikali ya Umeme Vijijini ya shilingi 100 kwa unit moja badala ya shilingi 2,000/- mpaka 3,700/- iliyokuwa ikitozwa na kampuni hiyo.

Akizungumza na wanakijiji wa kijiji cha Kanoni kisiwani Maisome, Waziri Kalemani alieleza kuwa tayari Serikali imetoa bei elekezi ya umeme nchi nzima ambayo inasimamiwa na EWURA na ndio inayotumika na TANESCO katika kuuzia umeme wananchi hivyo ni vyema wawekezaji wote wakaifuata na kuizingatia.

Bei ya kuwauzia umeme wananchi ni moja ambayo inatumika na TANESCO na kusimamiwa na EWURA, hivyo naagiza Kampuni ya Jumeme iwashushie wananchi wa kijiji hicho bei na ifanane na ile inayotozwa na TANESCO katika maeneo mengine na huduma ziboreshwe, umeme usikatike mara kwa mara bila sababu za msingi” alisema Waziri Kalemani. 

Waziri Kalemani aliendelea kwa kuagiza kampuni hiyo yenye ofisi zake jijini Mwanza kuhakikisha inafungua ofisi za kuhudumia wateja katika visiwa hivyo kwa huduma za dharura ili kuboresha huduma kwa wateja wanaohudumiwa na kampuni hiyo katika visiwa hivyo. 

Naye Mwakilishi wa bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo ya Jumeme, Profesa Isack Safari, alipotakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji wa agizo hilo, alieleza kuwa tayari wameanza kulifanyia kazi kwa kushusha bei ya umeme mpaka kufikia bei elekezi ya Serikali kama ilivyoagizwa pamoja na kubadilisha Uongozi wa kampuni hiyo.

“Mheshimiwa Waziri, Kufuatia maelekezo yako uliyoyatoa mara kwa mara ya kututaka tuzingatie bei elekezi ya Serikali katika mauzo ya umeme tayar tumeyazingatia na hivi leo ulivyokuja kujiridhisha umekuta tayari tulishajipanga na tulishaanza kutekeleza maagizo hayo toka siku tutu zilizopita”, alisema Profesa Safari 

Waziri Kalemani alimalizia kwa kuiagiza TANESCO kuanza taratibu za kupeleka umeme wa gridi ya Taifa katika visiwa hivyo kwa kutumia Miundombinu inayopita chini ya maji ili kuwaondolea adha ya umeme wanayopata wakazi wa visiwa hivyo vilivyoko ziwa victoria vikilizunguka jiji la Mwanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments