Waziri Mkenda Aanza Mkakati Kupunguza Bei Ya Mbolea


 Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imeielekeza Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini (Export Permit) badala ya vibali hivyo kutolewa ofisi ya Waziri wa Kilimo.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mbolea (YARA) Ofisini kwake Jijini Dodoma

Ili kuongeza ufanisi zaidi wa utendaji Waziri Mkenda amesema kuwa vibali hivyo vitatolewa kwa njia ya mtandao (Online) badala yake Ofisi ya Waziri wa Kilimo itakuwa na jukumu la kupewa taarifa ya utekelezaji wa utoaji vibali uliofanywa na TFRA.

Waziri Mkenda amesema kuwa serikali ina matumaini makubwa na wafanyabiashara wa mbolea kwani inaamini kuwa kurahisishwa utolewaji wa vibali hivyo kutawaongezea kasi ya kuagiza mbolea nyingi itakayoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya wakulima wa ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa kufuatia uingizwaji mwingi wa mbolea nchini jambo hilo litaimarisha uwezekano wa upatikanaji wa mbolea kwa bei nafuu kwa wakulima jambo litakalopelekea kuongezeka tija na uzalishaji kwa wakulima.

Kuhusu gharama za usafirishaji wa mbolea kupitia barabara, Waziri Mkenda amesema kuwa atafanya mazungumzo na Hazina ili kuona uwezekano wa huduma za kusafirisha mbolea kama itawezekana kutoa VAT.

“Tumegundua kuwa kusafirisha mbolea kwa reli kunapunguza sana gharama kwahiyo tumehimiza mbolea isafirishwe kwa reli kwenda kaskazini kwa maana ya mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Manyara pamoja na kusafirishwa kwa reli kupitia njia ya kati mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Singida N.k na Tazara tutafanya hivyo” Amekaririwa Prof Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa ili kupunguza gharama za mbolea nchini serikali imeielekeza Mamlaka ya Mbolea TFRA kuhakikisha kuwa inaongeza muda wa zabuni ambao walikuwa wameutoa.

Kuhusu Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Waziri Mkenda amesema kuwa katika makubaliano ya kikao kazi cha wizara atatafutwa mtaalamu elekezi  kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam shule ya Biashara kukaa kwa kipindi cha miezi sita na kuishauri serikali nini kifanyike ili kuifufua taasisi hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo Ndg Nyasebwa Chimagu amesema kuwa Waziri wa Kilimo ameendelea kukutana na wadau wa mbolea nchini ili kuhakishisha kuwa wakulima wanaendelea kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara hivyo ili kufikia hatua hiyo ni lazima kuongeza matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima.

Amesema kuwa nchi mbalimbali duniani zinaitegemea bandari ya Dar es salam katika kusafirisha mbolea hivyo vibali vya usafirishaji wa mbolea kutolewa moja kwa moja na TFRA itaongeza chachu ya urahisishaji kwa wauzaji wa mbolea lakini pia kurahisisha upatikanaji wa mbolea kwa haraka.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments