KENANI KIHONGOSI ATEULIWA KUWA KATIBU MKUU WA UVCCM


Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM, Kenani Kihongosi ambaye ameteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kushika nafasi hiyo, Kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Singida.

*** 
Na Charles James, Michuzi TV

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM, imemteua Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Kenani Kihongosi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho UVCCM.

Kihongosi ameteuliwa kushika nafasi hiyo akichukua nafasi ya Raymond Mwangala ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha.

Akizungumza na Wandishi wa Habari jijini Dodoma, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka amesema maamuzi hayo yamefanyika leo kufuatia kikao cha kawaida cha Kamati Kuu kilichoketi leo chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Shaka amesema katika kikao hicho pia, Kamati Kuu imempitisha Shekha Mpemba Faki kuwa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Konde lililopo Kaskazini Pemba Visiwani Zanzibar katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadae mwaka huu.

" Kamati Kuu imemteua Ndugu Kenani Kihongosi kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, hii ni baada ya aliyekua Katibu Mkuu, Raymond Mwangala kuteuliwa kuwa DC wa Ngorongoro," Amesema Shaka Hamdu Shaka.

Pia Chama hicho kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kwa namna ambavyo wanafanya kazi vizuri huku wakitekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/25.

Kenani Kihongosi amewahi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Mkimbiza Mwenge na baadae aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Singida na leo Kamati Kuu kumteua kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Vijana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments