RAS MWALUKO AELEZA AJIPANGA KUPIGANIA ELIMU YA MTOTO WA KIKE


Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika jana Mkoani Singida.

Na Edina Alex Singida
Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Singida Bi. Dorothy Mwaluko amekabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake Dkt. Angelina Lutambi huku akiahidi kusimamia kidete elimu ya mtoto wa kike.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano hayo jana, Mwaluko pamoja na mambo mengine ameomba ushirikiano kutoka kwa watendaji wote mkoani Singida ili kusukuma kasi ya maendeleo lakini zaidi kuleta ustawi kwenye eneo la elimu na maboresho ndani ya sekta ya afya.

"Kitaaluma mimi ni mwalimu,na kipaumbele changu hasa ni masomo ya sayansi, natamani na nitasimamia kuhakikisha watoto wa kike wanasoma masomo haya kwa mafanikio makubwa",alisema katibu Tawala na akaongeza;

"Kwenye elimu msitarajie kunidanganya na atakayekwenda kinyume hatutaelewana,".

Aidha kwenye eneo la afya ameomba kila mtendaji kuwajibika ipasavyo ili matarajio ya wanasingida yazidi kudhihirika kupitia serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Lutambi ambaye kwa sasa amehamishiwa Mkoa wa Mbeya, pamoja na mambo mengine amemueleza Mwaluko kuwa hali ya uchumi wa Mkoa inaendelea kuimarika siku hadi siku.

Hata hivyo ameshauri kuwepo kwa msukumo mkubwa na usimamizi kwenye utekelezaji wa sheria ya fedha za serikali za mitaa hasa kupitia tangazo la serikali namba 286 la April 5, 2019 ambalo lilielekeza asilimia 10 ya fedha za mfuko wa Wanawake,Vijana na wenye ulemavu zitolewe ipavyo.

"Utoaji wa fedha hizo mpaka sasa bado haufanyiki kulingana na sheria inavyoelekeza, hivyo msukumo mkubwa na usimamizi vinahitajika sana ili kutoa fursa kwa makundi hayo kunufaika", alisema.
Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi kulia akimkabidhi nyaraka Katibu Tawala mpya wa mkoa huo Dorothy Mwaluko kwenye hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika jana Mkoani Singida.
Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika jana Mkoani Singida.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments