CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA (CBE) , BENKI YA AMANA WAINGIA MKATABA KUWAPA MIKOPO WANAFUNZI 'ELIMU FINANCING' | MALUNDE 1 BLOG

Wednesday, June 2, 2021

CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA (CBE) , BENKI YA AMANA WAINGIA MKATABA KUWAPA MIKOPO WANAFUNZI 'ELIMU FINANCING'

  Malunde       Wednesday, June 2, 2021

Makamu Mkuu wa Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE) upande wa taaluma ya utafiti na ushauri wa kitaalamu Profesa Edda Lwoga akizungumza na waandishi wa habari.
Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Chuo Cha CBE kampasi ya Mwanza Gordian Bwemelo, wa pili Kushoto ni Makamu  Mkuu wa Chuo hicho wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Amana Benki
Katikati ni Meneja wa Benki ya Amana Shabani Diwani akiwa na wafanyakazi wenzake wakiwa wamekaa kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Chuo Cha CBE kampasi ya Mwanza

**

Na Hellen Mtereko,Mwanza
Kwa mujibu wa takwimu ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Mwanza mwaka jana kati ya wanafunzi 2660 waliokuwa wameomba kujiunga na masomo katika ngazi ya Cheti na Diploma ,zaidi ya Wanafunzi 1000 walishindwa kujiunga  kutokana na changamoto ya ukosefu wa ada.

Kupitia  changamoto hiyo chuo hicho kimeingia mkataba wa mwaka mmoja na Benki ya Amana kupitia mradi unaojulikana 'Elimu Financing' kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi ambao watakuwa hawana uwezo wa kulipa ada.

Akizungumza na waandishi wa habari leo  Juni 2,2021 Ofisini kwake, Mkurugenzi wa Chuo cha CBE kampasi ya Mwanza, Gordian Bwemelo alisema mkataba huo utasaidia kutatua tatizo la ukosefu wa ada kwa Wanafunzi wao.

"Mwaka Jana tulikuwa na watahiniwa 884 kwa programu ya muhula wa Septemba Wanafunzi 114 waliahirisha kufanya mitihani kwa kutokamilisha ulipaji wa ada. Kwa hiyo kwa makubaliano hayo ya kuingia mkataba wa mwaka mmoja na Benki ya Amana, wanafunzi wataweza kutimiza ndoto zao za kimasomo bila kuwa na changamoto yoyote inayohusu fedha",alisema Bwemelo.

Alisema kuwa mikopo ya Benki ya Amana ni fursa kwa Wanafunzi wao kwani Bodi ya mikopo(HESLB) imekuwa ikitoa mikopo kwa ngazi ya Shahada na kuwasahau wa ngazi ya Cheti.

Aliongeza kuwa Chuo hicho kimefanikiwa kuanzisha masomo mapya kwa upande wa tawi la Mwanza yatakayoanza rasmi 2021/2022, masomo hayo ni Shahada ya Elimu ya Biashara katika ufundishaji wa masomo ya Biashara kwa shule za  Sekondari pamoja na Stashahada ya Tehama(ICT).

Kwa upande wake  Makamu Mkuu wa Chuo hicho,upande wa taaluma ya utafiti na ushauri wa kitaalamu  Edda Lwoga alisema kuwa Chuo Cha CBE kampasi ya Mwanza kina jumla ya Wanafunzi 1677,wanaume 873 huku wanawake wakiwa 804.

Alisema ujio wa Benki ya Amana katika Chuo hicho utakuwa wenye tija kwani Wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo pamoja na kuahirisha mitihani yao itakuwa ni fursa kwao kwa kupata fedha ambazo zitawasaidia kulipia mahitaji yanayotakiwa pindi wawapo chuoni.

 Meneja wa Benki ya Amana,tawi la Mwanza Shabaan Diwani alisema kupitia mradi wao wa 'Elimu Financing' walianzia kwa mkoa wa Mwanza mwaka 2019 na hadi sasa bado wanaendelea nao na wameshatumia sh milioni 360 kwa ajili ya kutoa mikopo ya Elimu.


Alisema kupitia mkopo wao wa Elimu Financing kwa Mkoa wa Mwanza tayari Kuna wanufaika 400 na baadhi ya walionufaika ni kutoka Shule za Sekondari za Taqwa,Thaaqaafa,Ibanda Islamic na Waja.

Alisema lengo lao kubwa  ni kuhakikisha wanatoa mikopo kwa Wanafunzi wasiojiweza ili uweze kuwasaidia kutimiza ndoto zao za kielimu.


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post