WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKOSHWA NA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA KUZALISHA VIFAA VYA UMEME 'AFRICAB' | MALUNDE 1 BLOG

Friday, June 18, 2021

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKOSHWA NA UWEKEZAJI WA KIWANDA CHA KUZALISHA VIFAA VYA UMEME 'AFRICAB'

  Malunde       Friday, June 18, 2021
WAZIRI Mkuu  Mhe. Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa kiwanda cha kuzalisha vifaa mbalimbali vya umeme cha AFRICAB kutokana na uwekezaji wake kwenye sekta ya nishati na kusisitiza umuhimu wa mamlaka za Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

Majaliwa ametoa pongezi hizo leo alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha AFRICAB kwa lengo la kuangalia uzalishaji wake ambapo pamoja na mambo mengine alisema uwepo wa kiwanda hicho nchini kimeisaidia Serikali kuondokana na gharama kubwa za uagizaji wa vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi zilizokuwa zinaigharimu Serikali.

Alisema uwekezaji wa kiwanda hicho, mbali na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama, pia umesaidia kuharakishwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme nchini ikiwemo ya REA hatua inayoendelea kuliletea maendeleo Taifa na hivyo kusisitiza haja ya wawekezaji hao kuendelea kuthaminiwa.

“Zamani fedha nyingi zilikuwa zinatumika katika kuagiza vifaa mbalimbali vya umeme kutoka nje ya nchi, kwa sasa vifaa vingi vinazalishwa hapa hapa nchini zikiwemo zinazozalishwa na kiwanda hiki, naami kadri siku zinavyokwenda uwekezaji huu utakuwa hivyo kuzidi kulilete tija taifa, kikubwa mamlaka zinazosimamia suala zima la uwekezaji kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wenye nia ya kutaka kuwekeza hapa nchini” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema miradi mingi ya umeme inayoendelea kutekelezwa hivi sasa hapa nchini imekuwa ikitumia transfoma pamoja na nyaya zinazozalishwa na kiwanda hicho cha AFRICAB suala alilosema kuwa limekuwa faraja kwa Serikali kutokana na kiwanda hicho kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kujiletea maendeleo.

Aidha mbali na uwekezaji huo, Mhe. Majaliwa pia aliupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwa mmoja wa walipakodi wazuri kwa Serikali kwa kubainisha kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikilipa kodi kiasi cha Sh Bilioni 2 kila mwaka huku kikitoa ajira rasmi kwa watu zaidi ya 1000 walioajiriwa katika maeneo tofauti.

“Serikali inawapongeza kwa hatua hii nzuri iliyotokana na uwekezaji huu na zaidi inawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kutaka kuja kuwekeza hapa nchini hasa kutokana na uwepo wa mazingira mazuri yanayofaa kwa uwekezaji”, aliongeza Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake Meneja masoko wa AFRICAB David Tarimo, alisema uongozi wa kiwanda hicho umepokea kwa furaha ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa mahali hapo kwa kuwa kutaendelea kukiongezea chachu kiwanda hicho kuongeza nguvu ya uzalishaji.

Alisema wao kama wawekezaji wazalendo hapa nchini jukumu lao ni kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta ya nishati nchini inakuwa yenye tija kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakawawezesha wananchi kuzitumia kwa muda mrefu.

Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni baadhi ya wananchi kuendelea kuamini bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi ambazo nyingi zimekuwa zikiingizwa kwa njia ya ‘panya’ na zaidi zikikosa ubora ikilinganishwa na bidhaa zinazozalishwa nchini hususani kutoka katika kiwanda hicho.


Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post