WAZIRI MKUU : WAHARIRI ZINGATIENI VIWANGO NA UBORA KATIKA UANDISHI WA HABARI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka  wahariri wa vyombo vya habari  wahakikishe wanazingatia weledi na maadili katika uandishi wa habari  ili umma uweze kupata habari zenye ubora.

Ametoa wito huo leo Mei 20, 2021 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 10 wa Jukwaa la  Wahariri na kongamano la kitaaluma, Mkoani Morogoro

Amesema kuwa utendaji unaozingatia weledi ni chachu ya kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na wamiliki wake.

“kaulimbiu yenu ya Vyombo vya Habari na Maendeleo inahamasisha uandishi wa uwajibikaji. Vyombo vya habari vinapaswa kutambua katika kila habari vinayoiandika kuwa nyuma yake kuna masilahi ya taifa. Visipofanya hivyo, upotoshaji unaweza kuigawa nchi yetu, kuhatarisha amani na mshikamano wetu”.

Aidha Waziri Mkuu ameviasa vyombo vyote vya  habari nchini kuhakikisha vinatanguliza Uzalendo, Utaifa na Maslai ya Nchi katika kufanya kazi “Mjenga Nchi ni Mwananchi. Hakuna mwingine zaidi yenu wa kulisemea Taifa letu”

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayewakwaza mwandishi wa habari wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Niwahakikishie kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yake na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha misingi ya habari nchini. Kwa upande wenu wanahabari zingatieni sheria za nchi, msitumie vibaya kalamu zenu kuwachafua watu kwa chuki binafsi”.

Akizungumzia ushirikishwaji wa vyombo vya habari, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi na vyombo vya habari na kuwashirikisha kikamilifu katika utekelezaji wa mipango mikubwa ambayo kimsingi hutekelezwa kwa mipango ya muda mfupi yaani kipindi cha mwaka mmoja mmoja.

“Katika kuandaa mkakati wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo wanahabari mtashirikishwa kama wadau wengine kwani kwa kufanya hivyo mtaweza kuufahamu na kuwaelimisha wananchi kikamilifu”.

Waziri Mkuu pia ameziagiza Wizara na Idara zote za Serikali ambazo hazijalipia matangazo zifanye hivyo mara moja ili kuviwezesha vyombo hivyo kujiendesha.

“Ikiwa tangazo limefuata utaratibu kuanzia upatikanaji wake hadi kuchapishwa linapaswa kulipiwa mara moja. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nataka muangalie tatizo liko wapi na lipatiwe ufumbuzi”

Kadhalika Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kukamilisha mchakato wa kuundwa kwa Bodi ya Ithibati ya Habari itakalofanya kazi ya kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kuwezesha uundwaji wa Baraza Huru la Habari 

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema kuwa  kupitia Wizara ninayoiongoza imeendelea kushirikiana vema na vyombo vya habari  ili kuviwezesha vyombo hivyo pamoja na waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao bila vikwazo huku wakizingatia Sheria, Kanuni, weledi na maadili ya uandishi wa habari.

“Wizara kupitia Idara ya Habari – MAELEZO imekuwa ikiwasiliana mara kwa mara na taasisi na vyama vya wanahabari kwa ajili ya kupeana ushauri, miongozo na namna bora ya kuisimamia tasnia na kuhakikisha vyama hivyo pamoja na wanahabari wenyewe wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi”.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania  Deodatus Balile amesema jukwaa hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na amepongeza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuyaishi maono yake ya kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari.


(Mwisho)
IMETOLEWA NA

OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments