DC MGEMA APONGEZA WAKALA WA VIPIMO 'WMA' KUSIMAMIA NA KUTOA ELIMU YA VIPIMO SAHIHI


Na Andrew Chatwanga ,Songea
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Pololet Mgema amewapongeza  Wakala wa Vipimo Tanzania(WMA) kwa kuendelea kusimamia na kutoa elimu ya vipimo sahihi kwenye makundi mbalimbali ya jamii ambayo huwajengea uelewa pindi wanapohitaji huduma za kununua bidhaa au kuuza hasa mazao na kuachana na mazoea ya matumizi ya vipimo vya kienyeji.

Pongezi hizo amezitoa wakati akifungua kongamano la siku moja la upataji wa elimu ya vipimo sahihi ambavyo hutumia mizani mbalimbali inayotambulika na Serikali , uliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea Mkoani humo.
 
 Akifungua kongamano hilo ambalo lilimehusisha makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wajasiriamali pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wa masoko ya Manispaa hiyo ambapo mada mbalimbali zinazohusiana na vipimo zimetolewa , amesema kuwa Wakala wa Vipimo Tanzania wamekuwa wakijitahidi kupita kutoa elimu juu ya matumizi ya vipimo sahihi.

 Mkuu huyo amewataka Wakala wa Vipimo Tanzania wazidi kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa jamii kutoka na kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya makundi hayajafikiwa kikamilifu hasa Vijijini jambo ambalo husababisha baadhi yao  kuendelee kutumia vipimo vya kienyeji kama Vilita,Dumla,Ndoo na Kakongo.

Amewataka washiriki waliyobahatika kupatiwa mafunzo hayo waende wakawe mabalozi wazuri wa kuzuia Vipimo vya kienyeji na badala yake wakasimamie vipimo sahihi vinavyotambulika na Serikali 

 Kwa upande wake kaimu  Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoani Ruvuma ,Nyagabona Mkanjabi amesema kuwa hadi sasa wameshapita kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya Mkoani humo huku baadhi ya maeneo kama Wilaya ya Mbinga na Nyasa bado kumekuwepo na changamoto kubwa ya utumiaji wa Vipimo vya kienyeji.
 
 Kaimu Meneja huyo amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto hizo lakini bado elimu hiyo itazidi kuendelea kutolewa hadi kila mwananchi atambue umuhimu wa kutumia vipimo sahihi vinavyotambulika na Serikali kwa lengo la kumlinda mnunuzi na muuzaji.

 Naye mmoja wa wafanyabiashara ambaye pia ni mwenyekiti wa soko kuu la Songea Dometi Ngwenga amesema kuwa changamoto inayowakabili baadhi ya wafanyabiashara ambao waliyowengi ni wajasiliamali wadogo wadogo  ni bei ya mizani kuwa juu jambo ambalo baadhi yao wanashindwa kuimudu na hatimaye kuendelea kutumia vipimo vya kienyeji.

Afisa huduma kwa wateja na utawala kutoka EWURA Mkoani Ruvuma Magreth Temba ambaye pia ni mmoja ya waliokuwa katika utoaji wa mada zinazohusiana na sekta hiyo kwenye kongamano hilo, amesema kuwa mwananchi kupatiwa huduma bora ni haki yake ya msingi hivyo kama hawaridhishwi na huduma zinazotolewa kwa jamii na Mamlaka zinazohusika wana wajibu wa kuhoji au kutolea taarifa katika sehemu husika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments