KAMISHNA YAMBESI AWATAKA WATUMISHI WA KADCO KUFANYA KAZI KWA WELEDI


Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (katikati) akisisitiza jambo kwa watumishi wa KADCO (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo yanayotolewa na Tume ya kuwajengea uwezo, kulia ni Dkt. Natu Mwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kilimajaro na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO, Bibi Christine Mwakatobe (kushoto). (Picha na PSC).
Wawezeshaji wa mafunzo kwa watumishi wa KADCO (kutoka kulia) Bibi Celina Maongezi (Katibu Msaidizi) na Bw. Fanuel Mwakibete wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bibi Shani Kimanga Meneja Rasilimali Watu wa KADCO pamoja na Watumishi wa KADCO wakimsikiliza mgeni Rasmi Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (hayupo pichani) akifungua mafunzo yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa KADCO- KIA. (Picha na PSC)
Watumishi wa KADCO wanaoshiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo wakiwa na wawezeshaji kutoka Tume ya Utumishi wa Umma wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (hayupo pichani) leo katika ukumbi wa mikutano wa KADCO Kilimanjaro. (Picha na PSC.)
Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa George Yambesi (wa pili kutoka kushoto) akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADCO) Dkt. Natu Mwamba (wa pili kutoka kulia), Bw.Bambumbile Mwakyanjala (kulia) Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti Tume ya Utumishi wa Umma na Bibi Christine Mwakatobe, (kushoto) Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa KADCO leo katika Ukumbi wa Mikutano wa KADCO-Kilimanjaro. (Picha na PSC).
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADCO) Dkt. Natu Mwamba (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo baada ya Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (wa pili kulia) kufungua mafunzo kwa watumishi wa KADCO yanayoratibiwa na Kitengo cha Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti (Tume ya Utumishi wa Umma) wengine ni Bibi Christine Mwakatobe, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji KADCO na Bw. Bambumbile Mwakyanjala mratibu wa mafunzo haya yanayofanyika KADCO. (Picha na PSC).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO, Bibi Christine Mwakatobe akimkaribisha Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe. George Yambesi (wa pili kushoto) katika ukumbi wa mikutano wa KADCO kufungua mafunzo ya watumishi wa KADCO yanayotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma, wengine ni Bw. Bambumbile Mwakyanjala Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti wa Tume, kulia ni Dkt. Natu Mwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kilimajaro. (Picha na PSC).

**

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa George Yambesi amewataka Watumishi wa Kampuni ya Uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (KADCO) kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Yambesi amesema haya leo Mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa KADCO kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na usimamizi wa Utendaji Kazi kupitia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS) yaliyoandaliwa na KADCO na yanatolewa na wawezeshaji  kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma.

Alisema, watumishi wa KADCO wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu  za Utumishi wa Umma kwa kufanya kilicho sahihi huku wakizingatia utaalamu, uaminifu na uwajibikaji katika utendaji kazi wao wa kila siku wakati wa utoaji huduma.

“Naipongeza Menejimenti ya KADCO kwa kuandaa mafunzo haya kwa Watumishi ambayo naamini yataboresha utendaji kazi wenu na uzingatiaji wa Sheria wakati wa ushughulikiaji wa haki na wajibu wenu na wa wengine wakati wa utoaji wa huduma katika uwanja wetu wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA). Ni muhimu wakati wote mkafahamu kuwa nyinyi ni Taasisi ya kibiashara, wakati wote mnatakiwa kwa mbele kiushindani ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ” amesema.

Mheshimiwa Yambesi amesema kuwa hakuna Haki isiyo na Wajibu, Waajiri wana wajibu wa kuhakikisha watumishi wa umma wanapata stahili zao zote za kiutumishi ambazo ni haki yao kwa wakati na watumishi wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ambayo ni haki ya Waajiri.

“Hivyo, ni muhimu kwa watumishi wa umma kupandishwa vyeo, kuthibitishwa kazini na kulipwa stahili zao mbalimbali kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Aidha, Watumishi wa Umma wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu, uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kupata stahili zao” amesema.

Kamishna Yambesi amesema miongoni mwa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma  ni pamoja na kutoa Miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma; Kupokea na kushughulikia rufaa za mashauri yaliyotolewa maamuzi na Mamlaka za Nidhamu;  Kuwezesha, kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa Umma wa ngazi mbalimbali ili uwe wa ufanisi na wenye kuzingatia matokeo.

Akizungumzia kuhusu OPRAS Mheshimiwa Yambesi amesema OPRAS ipo kisheria ni vizuri watumishi wa KADCO na watumishi wa umma wakaielewa vizuri ili kila mtumishi aweze kupimwa utendaji wake na  apate anachostahili kwa haki bila upendeleo na upandishwaji  cheo kwa mtumishi  kutokane na ufanisi wake katika utendaji wa kazi. 

Kwa upande wake,  Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendelezaji Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (KADCO) Dkt. Natu Mwamba amesema mafunzo haya yanafanyika kipindi ambacho KADCO inaandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano ijayo ni imani kubwa kuwa malengo ya Tasisi yatakayowekwa yatakuwa ni yenye kutekelezeka na mtiririko wake utakwenda vizuri hadi kwa wafanyakazi ili waweze kuweka malengo yanayopimika katika utendaji kazi wao.

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha mheshimiwa Yambesi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO, Bibi Christine Mwakatobe amesema anaishukuru Tume ya Utumishi wa Umma kwa kukubali kuja kutoa mafunzo haya. Mafunzo haya yanafanyika baada ya Tume kufanya ukaguzi wa masuala ya Rasilimali watu KADCO na kubaini uwepo wa baadhi ya mapungufu. Menejimenti ya KADCO  inatarajia mafunzo haya yatakuwa ni yenye tija na yataongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Amesema jumla ya watumishi 291 wanatarajia kushiriki katika mafunzo haya ya wiki mbili.

                                                   Imeandaliwa na:

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

TUME YA UTUMISHI WA UMMA

KADCO-KILIMANJARO

10 MEI 2021

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments