MABALOZI WANAOIWAKILISHA TANZANIA NJE YA NCHI WAHIMIZWA KUONGEZA JUHUDI ZA KUTAFUTA MASOKO


Mabalozi wanaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya Nchi wameelekezwa kujipanga, kushiriki na kutafuta fursa zitakazowezesha bidhaa mbalimbali za Tanzania kupata masoko ya uhakika katika nchi walizopo.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi wakati akizungumza na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi na kuongeza kuwa , Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatamka bayana juu ya diplomasia ya uchumi sambamba na kuimarisha sauti ya Tanzania na taswira yake katika medani ya uhusiano wa kikanda na kimataifa.

Prof. Kabudi ameongeza kuwa ili kufanikisha hilo Balozi zinapaswa kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika jumuiya nyingine za kimataifa zikiwemo, Indian Ocean Rim Association, Indian Ocean Tuna Commission, South South Commission, South West Indian Ocean Fisheries Commission.

Aidha amewataka Mabalozi hao kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyoyatoa wakati akizundua Baraza la Wawakilishi ya kutaka Uchumi wa Bluu kupitia uvuvi wa Bahari Kuu unakuwa na manufaa kwa Wananchi hususani katika kuongeza mapato, ajira na kukuza uchumi kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni ya Muungano.

Pia Prof. Kabudi amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) katika maendeleo ya Taifa na kuzielekeza Balozi zianze na ziboreshe kanzi data ya Diapora ikiwa ni pamoja na kuwahimiza kuanzisha Jumuiya zao.

“Natambua kazi hiyo inaendelea na kwa sasa tuna data za diaspora takriban 98,658 na kuna jumuiya 77 za diaspora. Nichukue fursa kusisitiza umuhimu wa Balozi zetu kuboresha na kuharakisha zoezi hili kwa kubuni njia mbalimbali za kuwaandikisha”. Amesema Prof. Kabudi

Mkutano huo wa Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi umehudhuriwa pia na Naibu Waziri, Mhe William Tate Ole Nasha, Katibu Mkuu Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments