DC Iramba Aipongeza Wizara Ya Maji


 Na Mohamed Saif
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula ameipongeza Wizara ya Maji kwa kufikisha huduma ya majisafi na salama katika kijiji cha Songambele Wilayani Iramba.

Ametoa pongezi hizo Machi 16, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji unaonufaisha zaidi ya wananchi 6,000 wa Kijiji cha Songambele Mkoani Singida.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi, Luhahula alisema Wizara ya Maji imefanya jambo jema kutambua na kuipatia ufumbuzi kero ya upatikanaji wa majisafi iliyokuwa ikiwasumbua wanachi wa kijiji hicho.

“Wizara ya maji tunawapongeza sana, mmetambua changamoto ya iliyokuwa ikiwasumbua wananchi wa hapa na mkawaletea mradi, hili ni jambo jema sana, nawaomba mfike na maeneo mengine yenye changamoto kama ilivyokuwa hapa,” alisema Luhahula.

Akizungumzia mradi, Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Iramba, Mhandisi Ezra Mwacha alisema ulianza kutekelezwa Mei 1, 2020 na ulikamilika rasmi Novemba, 2020 na kwamba umetekelezwa na wataalam wa ndani kwa gharama ya shilingi milioni 168.6

Mhandisi Mwacha alisema mradi huo umewezesha kupunguza magonjwa yatokanayo na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama yakiwemo ya homa ya matumbo na kichocho.

“Mradi huu uliyozinduliwa leo utaimarisha hali ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa hapa na pia utaboresha suala zima la usafi wa mazingira wa maeneo yanayozunguka mradi,” alisema Mhandisi Mwacha.

Aidha, Mhandisi Mwacha aliishukuru Serikali ya Rais. Dkt. John Pombe Magufuli kwa dhamira yake ya dhati ya kumkomboa mwanamke hususan kwa kutoa fedha ya ujenzi wa mradi kwa wakati.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dr. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji ili kutimiza adhima yake ya kumtua mama ndoo kichwani na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” alisema Mhandisi Mwacha.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa mradi wa maji wa Songambele unakwenda sambamba na uzinduzi wa miradi na uwekaji wa jiwe la msingi maeneo mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka 2021 inayoanza leo Machi, 16 hadi Machi 22, 2021.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post