BILIONI 1.6 ZATOLEWA KWA AJILI YA KUHUISHA CHUO CHA TAIFA CHA SUKARI


Katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa sukari; Mfuko wa Maendeleo wa Tasnia ya Sukari (SIDTF) umeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kugharamia huduma za mafunzo, uendeshaji wa shughuli za Chuo cha Taifa cha Sukari pamoja na ununuzi wa vifaa vya mafunzo na ukarabati wa majengo.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu; Wizara ya Kilimo  Gerald Kusaya wakati wa kikao chake na Wadau wa tasnia ya  sukari  ikiwemo Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo, Wakulima wakubwa na wadogo wa miwa na Wazalishaji sukari katika ukumbi wa mikutano wa Wizara, Jijini Dodoma leo tarehe 5 Machi, 2021.

Katibu Mkuu Kusaya amesema ukosefu wa Wakufunzi, uchakavu wa vitendea kazi vya kuendesha mafunzo na kuchakaa kwa miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Sukari (National Sugarcane Institute – NSI) kulisababisha kusimama kwa utoaji wa mafunzo ya kilimo cha miwa na uzalishaji sukari kwa muda mrefu.

Katibu Mkuu Kusaya amesema kuwa juhudi za Serikali na Wadau wa tasnia ya sukari za kuimarisha Chuo cha Taifa cha Sukari zimeshaanza na kwamba zinaendelea kufanyika ili Chuo hicho kiwe bora na kinachotoa mafunzo ya kilimo cha miwa na uzalishaji sukari nchini.

“Chuo cha Taifa cha Sukari nchini ndiyo Chuo pekee cha Afrika Mashariki na Kati kitakachokuwa kikiandaa Wataalam wa teknolojia ya sukari na kinatariwa kurejea katika kutoa mafunzo Mwezi Septemba 2021 na tutarajie mabadiliko makubwa.” Amesisitiza Katibu Mkuu Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa juhudi za Serikali na Wadau zimewezesha Chuo cha Taifa cha Sukari kupata kibali cha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kutoa mafunzo kwa Ngazi ya Astashahada na Shahada ya kilimo cha miwa (Sugarcane technology) na uzalishaji wa sukari (Sugar technology).

Naye Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sukari Bwana Aloyce Kazimili  amesema kwa sasa tayari kuna Walimu ambao wanatoa mafunzo hayo lakini hawakusomea taaluma ya kilimo cha miwa kwa sababu hiyo  Walimu hao ni vyema wakasomeshwa na Serikali kwenye eneo hilo ili rahisi wao kuajiriwa mara kibali cha ajira kitakapotolewa.

Katibu Mkuu Kusaya amemuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo kuwapa uhamisho wa muda Watumishi wawili wa Kitengo cha Ugavi na Manunuzi na Mkaguzi wa Ndani ili irahisishe hatua za awali za kuhuisha uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Sukari pamoja na mambo mengine amewahidi Wadau wa mkutano huo kuwa atahakikisha ukarabati unaanza mara moja kwa kutumia Wataalam wa ndani na kwa mvumo wa “force account”.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post