TGNP KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI MWEZI MZIMA...HII HAPA RATIBA YOTE MIKOA 9Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Lilian Liundi


Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)kwa kushirikiana na wadau wake katika ngazi ya jamii na ngazi ya taifa,  wanaratibu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka mnamo tarehe 08 Machi. Maadhimisho haya ni ya kipekee katika harakati za Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi, kwani kwa namna ya kipekee wanawake na wadau wanaotetea haki za wanawake huja pamoja kusherekea mafanikio waliyofikia, kutafakari changamoto zinazoendelea kuwakabili na kupanga mikakati ya jinsi ya kuzitatua kwa kutumia fursa zilizomo katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, vikundi na kitaifa (kimfumo).

Kwa mwaka huu,  kauli mbiu ya kidunia ya siku ya wanawake duniani inasema “Wanawake katika Uongozi: Fanikisha Usawa katika Dunia yenye COVID-19”.  Kitaifa, Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: Wanawake Katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa”.

Kwa namna ya kipekee, tumejipanga kufanya maadhimisho haya ya siku ya wanawake duniani kwa kipindi cha mwezi huu mzima wa tatu tukiongozwa na mada kuu ya kidunia na kitaifa, ambapo ujumbe wetu mkubwa ni “Badili Mitazamo kuleta Usawa”na kwa vile lengo kuu ni kuangazia wanawake katika uongozi, tunaongozwa na msemo wa #ViongoziTuwaandaeSasaKwa ujumla, maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani yanalenga:

·       Kutambua na kusherekea mafanikio ya wanawake katika kupambana na mifumo isiyo Rafikikatika sekta mbalimbali

·       Kuweka mikakati yenye lengo la kuongeza idadi ya wanawake kwenye nafasi za uongozi wa aina mbali mbali-kisiasa, sekta binafsi, ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na Tanzania yenye usawa wa kijinsia

·       Kujadili kwa kina umuhimu wa kuthamini mchango wa mwanamke ndani ya jami na zaidi kuangazia ongezeko la kazi zisizo na malipo na kuweka mikakati ya kupunguza mzigo huo wa kazi kwa wanawake

·       Kuongeza mijadala katika Jamii juu ya simulizi na kauli zisizojenga na zisizo na tija kwa ustawi wa wanawake na maendeleo ya Jamii na ufanya ushawishi kwa jamii ili kuongeza ushiriki wao katika kujenga simulizi chanya na zenye tija kwa wanawake na Jamii kwa ujumla

·       Kuhakikisha kuwa maeneo muhimu yanayozalisha maarifa na ujuzi,yanaweka mazingira muhimu ya kumjenga ewezo na kujiamini mtoto wakike kama sehemu ya maandalizi ya kuwa kiongozi wa baadae. #ViongoziTuwaandaeSasa

Jumla ya matukio makubwa matano yatafanyika katika mwezi huu mzima wa Machi kama sehemu ya kuadhimisha siku ya Wanawake duniani.  Matukio hayo ni:

·       Ziara ya kwenye vyombo vya habari katika ngazi ya kitaifa na kijamii kuanzia tarehe 5-30 Machi 2021. Ziara hizi zinalenga kuendelea kutoa elimu kwa Jamii na kuibua mijadala itakayopelekea Jamii kuchukua hatua kuelekea mabadiliko chanya

·       Uzinduzi rasmi wa mikakati yetu kuelekea siku ya Wanawake Duniani kwa vyombo vya habari tarehe 6 Machi 2021.

·       Maadhimisho katika ngazi ya jamii “Dunia tuitakayo kwa wanawake na watoto wa kike” (The Future We Want for Women and girls)– Tarehe 7-20 Machi 2021

ü  TGNP kwa kushirikiana na Vituo vya Taarifa na Maarifa katika Halmashauri 18 katika mikoa 9 nchini tutafanya maadhimisho haya katika ngazi ya jamii ili kutambua na kusherekea wanawake walioleta mabadiliko na maendeleo katika maeneo yao.

ü  Kupitia maadhimisho haya tutaweza kuandika na kuweka kumbukumbu ya wanawake mashujaa katika ngazi ya jamii kutoka kwenye halmashauri hizo, ambao wataibuliwa na wanajamii wenyewe.

ü  Wanavituo vya Taarifa na Maarifa pia wataunganishwa na vyombo vya habari ngazi ya jamii ili kuweza kuujulisha umma juu ya ajenda yao ya kuwatambua na kuwasherekea wanawake hao ili kuleta chachu kwa wanajamii ndani na nje ya maeneo yao; kutambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo na hivyo, kubadili mitazamo yao juu ya uongozi wa wanawake, hivyo, kuweza kuongezaushahidi ni kwa nini umma, wake kwa waume wanapaswa kuhakikisha wanawake wanaongezeka katika nafasi za uongozi ili kuongeza chachu ya mabadiliko na maendeleo katika taifa letu na dunia kwa ujumla.

 

·       Kilinge cha Simulizi – tarehe 10 Machi 2021

ü  TGNP imekuwa ikiratibu Kiilinge vya simulizi tangu mwaka 2017 ambapo kimekuwani jukwaa mahususi linalowaleta pamoja vijana, wanafunzi na wanaharakati/ viongozi waliobobea katika Nyanja mbalimbali wakimwemo wanawake walio katika sekta zilizo na wananume wengi zaidi,ili kubadilisha uzoefu na kujifunza kutokana na simulizi za safari zao hadi kufikia walipofika.

ü  Kilinge hiki kitatumika kama sehemu ya kuwalea watoto wa kike kujiandaa kuwa viongozi na kuhamasika kuingia katika tasnia za sayansi na technolojia ambazo zinaaminika kuwa ni za wanaume.

·       Kampeni ya Kubadili namna ambavyo jamii imekuwa ikieleza kuhusu mwanamke (Changing Naratives) tarehe 11 Machi 2021.

ü  Kama sehemu ya muendelezo wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, TGNP kwa kushirikiana na WFT na TAMWA,tunaandaa mjadala utakaofanyika mtandaoni mwenye lengo la kubadili simulizi hasi katikajamii ambazo zinadhalilisha, kuwanyong’onyesha na kuondoa utu wa mtu, thamani yake na ujasiri wake.

ü  Mjadala huo unategemea kuleta pamoja washiriki mbalimbali wakiwemo vituo vya taarifa na maarifa, wasanii wa kike na wa kiume, wakilishi kutoka vyombo vya habari, wahamasishaji wa mitandao ya kijamii, wawakilishi kutoka TCRA, vinara wa jinsia wanaume wakiwemo wabunge.

·       Kongamano la pili Wanawake na Uongozi (Women and Leadership Summit) tarehe 16-17 Machi 2021

ü  Kongamano la kwanza lilizinduliwa rasmi na TGNP mwaka 2018 kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na nafasi za kufanya maamuzi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

ü  Kongamano la Wanawake na Uongozi ni jukwaa linaloleta kwa pamoja wanawake viongozi mahiri na wanawake viongozi chipukizi au wanaotia nia ya kuwa viongozi wakiwemo vijana wa kike ili kuweza kubadilishana mawazo na kujifunza kwa lengo la kuongeza wigo wa ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.

ü  Kongamano hili la Pili linatarajiwa kuwaleta pamoja viongozi mbalimbali katika siasa, uchumi kwa lengo la kushirikisha uzoefu, kuwezeshana na kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya wanwake viongozi katika majukwaa hayo.

·       Ziara ya Vijana katika vyuo vikuu kuanzia tarehe 20-24 Machi 2021:

ü  Kwa kushirikiana na Jukwaa la Vijana wa kike wanaharakati (YFF), tunatarajia kuwa na ziara katika vyuo vikuu vya nne vilivyopo Dar es salaam (Chuo kikuu cha Dar es salaam, Mzumbe, Mwalimu Nyerere na IFM) ili kutambua na kusherekea uongozi wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi wa wanafunzi hasa kwa wale wanawake walioweza kushika nafasi za urai au makamu wa rais katika serikali ya wanafunzi kwenye vyuo hivyo.

ü  Pia, katika ziara hizi, tutaweza pia tambua michango ya vijana walioweza kuhamasisha mabadiliko katika jamii.

ü  Kubwa zaidi ni kuendelea kuvuta vijana kujiunga na kukwaa hili wakiwa vyuoni lakini pia, kuanzisha majukwaa kama haya wakiwa katika maeneo wanayoishi ili kuleta mabadiliko katika jamii wanazotoka. Katika maadhimisho haya vijana hawa watakuwa na ujumbe mbalimbali watakaofikisha kwa jamii pia kwa njia ya mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

ü  Kupitia ziara hizi pia, vijana hawa wataweza kuhamasisha uundwaji wa vitovu ya jinsia vyuoni vyenye lengo la kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo Jinsia na maendeleo.

 

Tunapozungumzia ushiriki wa wanawake katika uongozi tuangalie katika mapana yake. Jinsia ni suala la Maendeleo hivyo hatuna budi kwa pamoja kutoa kipaumbele ili kuongeza ushiriki wa wanawake wenye tija katika Maendeleo. Ni kwa mantiki hii TGNP tumeamua kuandaa matukio hayo niliyoeleza hapo juu kama sehemu ya kutoa fursa kwa wanawake na wadau wengine kutafakari wapi tumefanikiwa, wapi bado kuna changamoto na kupanga mikakati ya kuimarisha ushiriki wa wanawake katika ngazi zote za maamuzi pamoja na uongozi.

 

TAKWIMU:

Takwimu za IPU (2019) zinaonesha kuwa hadi Januari 2019, wanawake wakuu wa nchi (Head of state) walikuwa 10 kati ya 152 (asilimia 6.6) tu ambapo wanawake wakuu wa Serikali (head of government) walikuwa 10 kati ya 193 (asilimia 5.2). Kwa upande wa Afrika kwa sasa kumekuwa na marais wanne wanawake, aliyekuwa rais wa Malawi, Joyce Hilda Banda (Aprili 2012- Mei 2014), aliyekuwa rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf (Januari 2006-Januari 2018), aliyekuwa raisi wa Mauritius Ameenah Gurib-Fakim (June 2015- March 2018) na Rais kutoka Ethiopia Sahle-Work Zewde (Octoba 2018 hadi leo).

Vile vile, takwimu zinaonesha kuwa hadi January 2019, kidunia maspika wabunge wanawake ni asilimia 19.7 na manaibu speaker wanawake ni asilimia 28.2. kulingana na ripoti hiyo hiyo, Wabunge wanawake katika nchi zote walikuwa ni asilimia 24.3. ambalo ni ongezeko la asilimia 13 kutoka asilimia 11.3 mwaka 1995. Pia kufikia 2020 kulikuwa na wastani wa wabunge wanawake 24.4%. katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ambalo ni ongezeko la asilimia 14.6 tangu mwaka 1995.

 

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofanya vizuri katika ushiriki wa wanawake katika uongozi. Kulingana na takwimu za Interparliamentary Union (IPU) hadi 2020, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa nchi za Afrika Mashariki na nafasi ya 23 duniani kwa kuwa na 36.9% ya wanawake wabunge ambapo Rwanda imeshika nafasi ya kwanza hadi kidunia kwa kuwa na 61.3%. Hata hivyo, bado hatujaweza kufikia 50/50 na hivyo, hatuna budi kuongeza juhudi katika kuongeza nafasi za wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi ili kufikia malengo.

Kwa Tanzania, kwa mara ya kwanza baaada ya uhuru tumeweza kuwa na mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa raisi Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameweza kushika nafasi hiyo kwa awamu mbili mfululizo toka 2015-2020 na awamu hii ya 2020-2025. Hii ni hatua ya kupongezwa katika nchi yetu.  Vile vile kwa mara ya kwanza katika nchi yetu bunge la 10 tumeweza kupata spika wa Bunge mwanamke Mhe. Mama Anne Makinda na katika bunge la 11 na la 12 tunaye naibu Spika wa bunge Mhe. Dr Tulia Akson. Hata hivyo katika kamati za Bunge uwakilishi wa wanawake   kama wenyeviti wa kamati ni mdogo sana.  Kwa upande wa wabunge wa kuchaguliwa, wanawake ni 25 ya wabunge 264 wa kuchaguliwa ambayo ni sawa na asilimia 9.5% tu ya wabunge wote; idadi ya wabunge wanawake wa viti maalumu ni 113 ambayo ni sawa na asilimia 29 ya wabunge wote.  Jumla ya wabunge wanawake ni 142 sawa na asilimia 37 ya idadi ya wabunge wote ambao ni 393.  Hii bado ni idadi ndogo ukilinganisha na lengo la kufikia asilimia 50/50.

Uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi wa kisiasa katka ngazi ya udiwani bado ni changamoto kubwa. Licha ya juhudi za wadau mbalimbali ambazo zinafanyika ikiwemo seriali asasi za kirai na wadau wa Maendeleo. Takwimu zinaonesha kuwa (NEC, TEMCO) kwamba idadi ya madiwani wanawake wa kuchaguiwa kutoka kwenye kata ni 204 ambayo ni sawa ana asilimia 5 ya madiwani wote. Madiwani wanawake wa viti maalumu ni 1,611 Sawa na asilimia 30 ya madiwani wote. Kwa ujumla wanawake madiwani ni 1,815 sawa na asilimia 33.9 ya madiwani wote.  Madiwani wa kuchaguliwa ndio wenye fursa za kugombea na kushika nafasi ya mwenyekiti wa halmshauri ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa mkutano mkuu wa baraza la madiwani la Halmashauri ambalo lina mamlaka ya kujadili na kupitisha bajeti ya halmashauri.  Kwa bahati mbaya ushiriki mdogo wa wanawake madiwani wa kuchaguliwa unawanyima wanawake wengi kushika nafasi za uenyekiti wa halmashauri. Tanzania bara ina jumla ya halmashauri 185 ambapo ni Halmashauri 6 tu sawa na asilimia 3.2 ambazo zinaongozwa na wawanake wenyeviti.

Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanaishi katika ngzi ya vijini na kata na chimbuko la maendeleo ya nchi ni katika ngazi hiyo. Hivyo, ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi hizo muhimu na za kimkakati ni changamoto katika kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi na endelevu.

Ikumbukwe kuwa serikali yetu imeridhia mikataba na matamko mengi ya kuleta Usawa wa Jinsia  na Maendeleo katika ngazi za kimataifa na kikanda.; yakiwemo:Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR:1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979), Mpango Kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo, na Mkataba wa Hiari wa Jinsia na Maendeleo kusini mwa Africa (SADC Gender and Development Protocol,) mikataba hii inaelekeza serikali husika kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi sawa na wanaume katika ngazi mbalimbali za uongozi. Vile vile Tanzania Dira ya Maendeleo ya 2025 (TDV 2025) imetambua kuwa mojawapo ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi ni pamoja na jamii yenye muono wa kimaendeleo ambapo pamoja na mambo mengine unakuwa na tamaduni wezeshi hususani kwa wanawake na makundi mengine.

Licha ya juhudi hizo za kuridhia matamko na mikataba bado wanawake wanakutana na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha Maendeleo yao hasa ushiriki wao katika nafasi za maamuzi. Tofauti za utajiri na za kijinsia zinaongezeka, katika nchi zinazoendelea zikiwa na ufinyu wa utajiri, maarifa na teknolojia. Wanawake maskini wa mijini na vijijini wanazidi kusukumwa pembezoni, wakionekana kama siyo sehemu ya jamii. Tafiti zinaonesha kwamba nchi za Afrika zinapoteza takribani dola za kimarekani 105 milioni kwa mwaka  kwa kutowaingiza wanawake katika uchumi.  Pia takwimu zinaonesha kuwa wanawake ni zaidi ya asilimia 70 ya wakulima wadogo ambao ndio wanalisha nchi yetu. Wanawake walioko katika sekta isiyo rasmi ni asilimi 51.1% ambapo wanaume ni 48.9%.  Vile vile ni 20% tu ya wanawake wanamiliki ardhi. Ufikiaji wa huduma za jamii bado ni changamoto hususan kwa wanawake kwani licha ya jitihada za kumtua mama ndoo Kichwani bado vijijini wanawake wanatumia muda mwingi kati ya masaa 3 hadi 5 kutafuta maji. Huduma za afya, hasa afya ya uzazi ni changamoto kwani bado wanawake wanakufa kwa wingi kwa vifo vya uzazi kati ya vizazi 100,000 tunapoteza wanawake 556, kwa upande wa elimu pamoja na kupongeza jitihada za elimu bure bado watoto wetu wa kike wanashindwa kuhudhuria masomo kwa kukosa vifaa na mazingira ya kujihifadhi wakati wakiwa katika siku zao za mwezi.

Kwa mawasiliano zaidi:Wasiliana nasi kupitia idara ya mawasiliano na habari

1.     Monica John

Simu: 0652 267 611

Barua Pepe: monica.john@tgnp.or.tz

2.     Jackson Malangalila

Simu: 0657 479 490

Barua Pepe: jackson.malangalila@tgnp.or.tz

3.     Asteria Katunzi

Simu: 0711 407 222

Barua Pepe: Asteria.katunzi@tgnp.or.tz

 

Soma pia :

MATUKIO MBALIMBALI YANAYOFANYWA TGNP INAPOADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2021


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post