WAHARIRI VYOMBO VYA HABARI WAKOSHWA NA MFUMO WA GEPG


 Na. Peter Haule na Ramadhani Kissimba, WFM, Arusha
KATIBU Tawala Mkoa wa Arusha Richard Kwitega ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali kwa ujumla kwa kuweka mfumo imara wa ukusanyaji mapato ya Serikali wa GePG ambao unawawezesha wananchi kulipia huduma mbalimbali za Serikali kupitia mfumo huo.

Akizungumza wakati akifungua semina ya siku mbili kwa Wahariri kutoka Vyombo mbali mbali vya Habari nchini kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, iliyoanza leo jijini Arusha, amesema kuwa mfumo wa GePG umeimarisha ukusanyaji mapato ya ndani na kuwezesha mwananchi kuwa na uhakika wa malipo mbali mbali yanayofanyika kupitia ( Control Number) ambayo ni salama zaidi katika mchakato wa ukusanyaji mapato.

Amesema, mfumo huo pia unawezesha wananchi kuokoa muda kuanzia anapopata Ankara zake, namna ya ulipaji wake, na upatikanaji wa Stakabadhi yake ikiwa ni pamoja na fedha kufika Serikalini kwa wakati na kuepuka upotevu wa mapato ya Serikali.

’’Mfumo huu wa GePG umeimarisha  ukusanyaji mapato kwa   kuondoa  gharama za miamala ya fedha kwa Umma, utaratibu usio rafiki wa ulipaji huduma za Umma pamoja na makusanyo yote kuonekana kwa uwazi na uhakika wa taarifa mbali mbali." Amesema Kwitega.

Aidha, alisema kuwa, mfumo huu umeweza kuongeza mapato mfano Wakala wa misitu Tanzania walikuwa wakikusanya kiasi cha shilingi bilioni 95 kwa mwaka kabla ya mfumo huu wa GePG lakini baada ya kutumia mfumo huo waliweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni.115.

Vile vile, alisema kuwa Shirika la Umeme TANESCO liliweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 38 kwa mwwaka  ambazo zilikuwa  zikitumika  kulipia gharama za wakala kabla ya mfumo huo ambapo baada ya kufunga mfumo huu wameweza kuokoa fedha hizo ambazo zilikuwa gharama za miamala kwa umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango  Bw. John Sausi amewataka wahariri kuhakikisha kuwa wanatoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa  kutumia mfumo wa Serikali wa  Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato(GePG)  katika kufanya malipo ya huduma mbalimbali za Serikali .  Sausi amesema, kabla ya mfumo huo wa GePG kulikuwa na upotevu mkubwa  wa mapato ya Serikali   kutokana na kutokuwepo kwa uwazi wa ukusanyaji wa mapato pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi na kwa wakati.

“Niwaombe wahariri muwaeleze wananchi kuepuka kulipa pesa taslimu kwa kuwa, kwanza hazitafika kwa wakati pili zitapotea na mwananchi ataingia hasara ya kulipa kwa mara nyingine tena, hivyo watumie 'Contorl Number' ili kuepuka upotevu usio wa lazima.”amesema John.

Aidha  alisema kuwa Mfumo huo umeunganishwa na Taasisi mbalimbali za Serikali za mitaa, Halmashauri, Taasisi na serikali kuu zipatazo 670.

Bw. Sausi alisema mfumo huo ulianzishwa rasmi mwaka 2017 kwa Taasisi chache ambapo umewezesha  kuongezeka kwa mapato kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mchumi Mwandamizi anayesimamia mapato ya Serikali kutoka Idara ya Uchambuzi wa Sera Bi. Neema Maregeli alibainisha kuwa mfumo  wa GePG  umeongeza mapato ya Serikali kutoka wastani wa shilingi bilioni 800 kabla ya Mfumo huu  hadi wastani wa  trioni 2.4 kwa mwaka.

Alisema kuwa mapato haya yamewezesha Serikali kutekeleza shughuli zake  mbalimbali ikiwemo kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Vile vile ,  alisisitiza umuhimu wa  vyombo vya habari  kupitia wahariri walioshiriki mafunzo hayo kuwaelimisha wananchi kwa ufasaha  umuhimu wa kulipa kodi, kudai risiti wanapofanya manunuzi na kwa upande wa wafanya biashara kutoa risiti wanapouza huduma na bidhaa mbalimbali.

MWISHO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments