Majaliwa Aipa CEOrt Mbinu Kuvuna Watendaji Wakuu Wazawa


 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Jukwaa la Taasisi ya Wakurugenzi na wamiliki wa makampuni binafsi nchini (CEOrt) kushirikiana na serikali pamoja taasisi nyingine ili kubaini maeneo yenye uhitaji wa viongozi wakuu wazawa na kutoa mafunzo yenye tija.

Pia ameitaka Bodi ya wakurugenzi wa Jukwaa hilo kuandaa mipango ya mafunzo yenye lengo la kutambua na kujenga uwezo kwa Watanzania katika sekta za kipaumbele hususan sekta ya madini, mafuta na gesi, ujenzi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Majaliwa ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam katika mahafali ya wahitimu wa Programu ya Uanagenzi kwa Maofisa Watendaji Wakuu (CEO Apprenticeship Program).

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chuo cha Strathmore Business School (SBS) cha nchini Kenya, jumla ya washiriki 16 wamehitimu mafunzo hayo yaliyokuwa yameandaliwa na CEOrt kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha watanzania kushika nyadhifa za juu za Uafisa Mtendaji Mkuu (CEOs) na Ukurugenzi Mtendaji(MDs) katika makampuni na taasisi mbalimbali.

Waziri Mkuu alisema ushirikiano wa CEOrt pamoja na Taasisi ya Uongozi inayoendesha programu za mafunzo ya uongozi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Alto cha Nchini Finland, utaleta tija, kuondoa marudio na kuimarisha ubunifu katika kutoa mafunzo na kuleta manufaa kwa washiriki wa mafunzo hayo.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka CEOrt washirikiane katika kuwajengea uwezo wa wataalam wabobezi katika masuala ya uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka kwani yanaendana na falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya ‘hapa kazi tu’, pia yamekuja katika kipindi ambacho nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo viongozi hao watumie ujuzi na weledi katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miradi,” alisema.

Aidha, akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt, Sanjay Rughani alisema mafunzo hayo pia yamelenga kuwajengea wataalam wa kitanzania uwezo mkubwa ili waweze kushindana katika kuhudumu kwenye nafasi za utendaji mkuu katika taasisi, programu na miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa.

Alisema programu hiyo ilianza miaka miwili na nusu iliyopita, baada ya kufanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 60 ya viongozi wa kampuni mbalimbali wenyewe walitaka watanzania na waafrika wamiliki hizi nafasi za mkurugenzi mtendaji lakini kuwapata hawa Ma-CEOs ilikuwa kazi ngumu sana.

“Katika programu hii washiriki 16 ambao wamehitimu, wametoka kwenye kazi zao kama za ofisa rasilimali watu na nyingine lakini watatu kati yao wamepandishwa cheo na kuwa Ma-CEOs katika makampuni ya Songas, PASS na Access Benki.

“Kwa kweli nina furaha kubwa kwani nilikaa nao tangu siku ya kwanza ya mafunzo na sasa wanaweza kuzungumza mambo ya kidunia, kisera, kiuchumi na kuwezesha kampuni kupiga hatua,” alisema.

Aidha, mmoja wa wahitimu hao, Anna Shanalingigwa ambaye pia amepandishwa cheo katika kipindi cha mafunzo hayo na kuwa Kaimu Meneja Mkuu wa Asasi ya kusaidia sekta binafsi ya kilimo - PASS, alisema kufikia malengo hayo kunahitajika nguvu za ziada.

“Kwa sababu mwanamke hata kama una ufaulu mzuri kiasi gani kwenye masomo kuna nafasi ya mama na mke ambayo jamii inakutegemea uishikilie,” alisema.

Alisema ili kufikia malengo hayo, mwanamke anahitaji kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanaume, wafanyakazi na viongozi wake ili awe kiongozi bora kwa manufaa ya kampuni na jamii kwa ujumla.

Hoja hiyo pia iliungwamkono na mhitimu mwingine, Rayson Foya ambaye ni Mkuu wa idara ya uchumi katika benki ya Standard Charter.

Foya alisema kuhitimu kwake ni deni kwa watu anaowaongoza na jamii nzima.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post