AGIZO LA MAGUFULI KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI WA BI ELIZABETH MANYONI LATEKELEZWA 100%

 

Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) (aliyeshika  hati  ya ardhi) akiwa kwenye picha ya pamoja  na  Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi( mwenye msalaba), Viongozi wa  Wilaya ya Manyoni,wataalam wa ardhi  Mkoa  wa Singida na wanafamilia  mara baada ya kukabidhiwa hati hiyo ya eneo lake lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa  kwa Kampuni  mmoja ya simu za mikono ambapo  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza  lirejeshwe mara moja  kwa  bibi huyo ambaye ndiye ataingia  mkataba  wa upangaji na Kampuni  hiyo.

Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) akitoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  mara baada  ya kukabidhiwa  hati ya eneo lake.


Na John Mapepele, Manyoni

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ametekeleza agizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilomtaka kushirikiana na Viongozi wa Wilaya ya Manyoni kumrejeshea umiliki  wa eneo  lililokuwa mali ya  Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) ambaye lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa  kwa Kampuni  mmoja ya simu za mikono ambayo  imeweka mnara wa mawasiliano lirejeshwe mara moja  kwa mama huyo ambaye ndiye ataingia  mkataba  wa upangaji na Kampuni  hiyo.

Akikabidhi  hati ya umiliki wa ardhi wa miaka 66 wa eneo hilo la Majengo Kiwanja Na 13 hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Singida  Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano  inayoongozwa na Mhe, Dkt. John Pombe  Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi wanyonge ili wapate haki zao na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo ili kuchangia katika uchumi wa kati na hatimaye uchumi wa juu wa Taifa letu.

Amesema Mkoa umejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi inakwisha mara moja  kwenye Mkoa wa Singida na kuagiza Wakuu wote wa Wilaya na Wataalam wa ardhi  kuanzia sasa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo husika badala ya kufanya mashauri ya migogoro ya ardhi  maofisini.

“Kuanzia leo sitaki kuona shauri na migogoro ya ardhi ikitatuliwa  maofisini, naagiza wakuu wote wa Wilaya katika Mkoa wangu  na wataalam kwenda moja kwa moja  kutatua  migogoro ya ardhi ya wananchi  katika maeneo ya migogoro, hatua kali zitachukuliwa kwa wote ambao hawatatekeleza  agizo hilo” alisisitiza Mhe. Nchimbi

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni amesema ni lazima iishe mara moja kwa  kuwa Manyoni  ya sasa ni Sebule ya Makao Makuu ya nchi-Dodoma na kwamba watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wanakuja Manyoni kwa kuwa kuna maeneo mazuri yenye fursa za uwekezaji hususan kwenye  viwanda, biashara  na kilimo cha zao la Korosho ambapo kwa sasa Wilaya hii inaongoza siyo tu Tanzania bali katika  Bara la Afrika kwenye kilimo hicho ambapo kumekuwa na shamba la pamoja la Kilimo cha Korosho (Block Farming)lenye takribani ekari 25000.

“Haiwezekani Manyoni hii ambayo ni lango la makao  makuu ya nchi ikaendelea kuwa na migogoro ya ardhi ambapo sasa  ardhi yake imebeba uwekezaji mkubwa katika nchi yetu” aliongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa

 Akipokea hati yake ya umiliki wa eneo hilo, Bibi Elizabeth Msalali  alimshukuru Rais Magufuli kwa kusaidia kupatikana kwa kiwanja chake ambapo amesema Magufuli  ameonyesha kuwa ni Rais anayewapigania  watu masikini na wanyonge kama yeye hivyo anamwombea kwa Mungu azidi kumbariki katika utumishi na maisha yake kwa ujumla.

Aidha Mtoto wa pekee wa Bi Elizabeth ambaye ndiye aliyemwomba Mhe. Rais Magufuli kuingilia kati suala hili Bwana, Adamu Kazimoto alimshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuharakisha  kukamilisha  mchakato wa kupata  hati ya umiliki wa kiwanja  hicho kwa mama yake ambapo amesema  mchakato huo umechukua muda mfupi sana.

“Naomba niwe mkweli kama tungekuwa na fedha ya kulipia  hiki kiwanja  nadhani  ingechukua  siku  moja au mbili tu baada ya agizo la Mhe.Rais maana Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Dada Shamimu Hoza alikamilisha  utengenezaji wa hati hiyo mara moja baada ya tamko  hilo la Mhe.Magufuli jambo ambalo limetupa faraja kubwa kwani sasa mama yangu amepata  haki yake” ameongeza Adamu

Akifafanua Adamu amesema suala hili  alianza kufuatilia zaidi ya  miaka tisa iliyopita, na anamshukuru Rais Magufuli  kwa kutoa suluhisho la kudumu ambapo pia ameongeza kwamba mgogoro huo umeifanya familia ya Mzee Kazimoto kuwa kitu kimmoja licha sintofahamu ambazo zilikuwepo hapo awali kwa sababu ya tamaa ya pesa kwa wanafamilia.

Mhe. Rais John Pombe  Magufuli  alilitoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kushughulikia mgogoro  huo tarehe 31Januari 2021 aliposimama kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini akitokea Tabora kwenda Dodoma.

Rais Magufuli  alisikiliza  kero inayowakabili wananchi hao ambao walilalamikia  kitendo cha Idara ya Ardhi kuchukua maeneo  yao bila kuwalipa fidia  na wengine kuamriwa  kuondoka katika  eneo hilo baada ya kupewa nyaraka  za kupatiwa  radhi(offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo hilo na Idara ya Ardhi.

Rais ameagiza wananchi wenye offer waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa na wamiliki wa asili wa eneo hilo  kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria.

Awali, kufuatia agizo  la Mheshimiwa Rais, Timu Maalum ya wataalam kutoka Mkoani na Wilaya ya Manyoni iliyoongozwa na Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Shamimu Hoza Shaban ilikutana  familia nzima ya mmiliki wa asili wa eneo hilo marehemu  Salum Kazimoto aliyefariki mwaka 1973  ambayo   ilikuwa  inavutana  kuhusu  umiliki wa eneo  hilo ambapo  baada ya  majadiliano ilikubaliana kwa kauli mmoja kwamba mmliki halali  wa eneo hilo ni Bibi Elizabeth Msalali.

Kutokana  na  Wilaya ya Manyoni kuonekana kuwa na migogoro ya ardhi kadhaa ya ardhi kwa muda mrefu sasa, mkakati maalum wa kusikiliza kero hizo umeandaliwa  ambapo timu ya wataalam na viongozi wa Halmashauri hiyo unazungukia katika maeneo husika ili kuhakikisha migogoro yote inaisha  kama ilivyoamriwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments