CHUO CHA SAUT KUZINDUA SAUT ALUMNI MWEZI APRILI

 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha MT. Agustino cha Tanzania (SAUT) Balozi Professa Costa Ricky Mahalu (Katikati) akizungumza na Mwenyekiti mteule wa SAUT Alumni Ndugu Pius Lufutu (Kushoto) pamoja na Mwanasheria wa Chuo Padri Claudius Nkwera.

**

Na Mwandishi wetu, SAUT

Chuo kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kampasi ya Mwanza kinatarajia kuzindua umoja wa wanazuoni (Alumni) waliowahi kuhitimu chuoni hapo toka kuanzishwa kwake.

Hayo yamejiri hapo jana pindi viongozi wakuu wa chuo hicho walipokutana kwa ajili ya kikao cha awali kujadili uanzishwaji wa SAUT Alumni mnamo mwezi Aprili.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Mwenyekiti mteule wa umoja wa wanazuoni hao Pius Lufutu alisema uzinduzi rasmi wa Alumni ni kwa ajili ya kuwatambua wanazuoni wote waliowahi kuhitimu chuoni hapo pamoja na wao kushiriki katika kuendeleza chuo kupitia miradi mbalimbali.

“Uzinduzi wa Alumni hii itakuwa ni kwa ajili ya kuwatambua wanazuoni wote waliowahi kuhitimu chuoni hapa iwe wapo ndani ya nchi ama nje ya mipaka. Lengo likiwa ni kuwahamasisha kushiriki katika katika kuendeleza miradi itakayo chochea maendeleo ya chuo kama namna yao kuonesha fadhila,” alisema.

Aidha pamoja na hayo, Lufutu alisema chuo pia kitawasaidia Alumni hao kuwatafutia fursa mbalimbali pamoja na kushirikiana nao kwa ukaribu ili kuweza kuchochea maendeleo yao.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo SAUT, Balozi Professa Costa Ricky Mahalu alitoa wito kwa Alumni kuweza kuwa tayari kushiriki kikamilifu huku ikitarajiwa Alumni kuwa ni kwa ajili ya manufaa ya wote.

“Nina imani kabisa kwamba uzinduzi wa Alumni utawanufaisha wengi, ikiwemo pia kuisaidia jamii ya chuo chetu hiki. Hivyo ni wito wangu kwamba wanazuoni wahitimu watakuwa tayari kwa ajili ya kuking’arisha chuo chetu na kukifanya kuwa sehemu endelevu ya kupata elimu bora katika mazingira wezeshi,” alisema Profesa Mahalu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post