SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATUMISHI WANAOFANYA KAZI VITUO BINAFSI KATIKA MUDA WA KAZI


 Na WAMJW- Kilimanjaro
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya Afya imeanza kufuatilia Watumishi walioajiriwa na Serikali wanaofanya kazi katika vituo vya kutolea huduma za Afya binafsi katika muda wanaotakiwa kuwa katika vituo vyao vya Serikali.

Hayo yamesemwa jana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali za Watu Binafsi nchini wakati akiongea na Waandishi wa habari baada kikao na wajumbe wa Bodi hiyo ikiwani sehemu ya maboresho ya huduma za Afya nchini, Mkoani Kilimanjaro.

"Tumeanza kufuatilia Watumishi wa Umma wanaofanya kazi katika Hospitali binafsi muda wa kazi, mtumishi yeyote atakayethibitika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali pamoja na mmiliki wa kituo atakachokuwa akifanya kazi ndani ya muda wa kazi" amesema Prof. Makubi.

Aliendelea kusema kuwa, wamiliki wa Hospitali Binafsi wahakikishe kuwa wanazingatia na wanafuata Sheria, kanuni, miongozo na taratibu, za usajili wa vituo hivi ikiwemo watumishi wanaowasimamia.

Aidha, Prof. Makubi ameagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wafawidhi wa Vituo na Waratibu kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha kuwa vituo hivi vinafuata sheria za Utumishi wa Umma na za Hospitali Binafsi

Amesema, Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wafawidhi wa Vituo waweke na kusimamia mifumo ya kuhakikisha watumishi wa Umma wanakuwepo katika vituo vyao ndani ya saa za kazi.

Mbali na hayo amewaagiza Wamiliki wa vituo binafsi wahakikishe watumishi wa Umma hawafanyi kazi kwenye vituo vyao katika muda wa serikali, huku akisisitiza kuwa, yoyote atakayebainika kuvunja sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo.

Hata hivyo, amewakumbusha wamiliki wote wa vituo binafsi nchini kufanya kazi kwa kushirikiana na Bodi za usimamizi wa kutoa huduma za afya ili kuboresha huduma za bila kuvunja Sheria, kanuni, miongozo na taratibu zilizopo.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post