SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WADAU KUIKUZA BONGO FLEVA NCHINI


 Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dar es Salaam
Mashindano ya Bongo Star Search yamehitimishwa usiku wa kuamkia Januari 30, 2021 jijini Dar es Salaam ambapo Msanii wa muziki wa Kizazi kipya Yusuph Nizar ameibuka kidedea na kujinyakulia kitita cha Sh. Milioni 20 na kukabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya fedha hizo.

Akizungumza mara baada ya kutaja majina ya mshindi wa kwanza hadi wa watatu katika mashindano hayo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa Sanaa katika kuendeleza vipaji vya vijana hatua inayosaidia kuwaongezea kipato na kuboersha maisha yao.

“Dhamira na malengo ya Serikali ni kusaidia Bongo Fleva iwe fani kubwa ndani na nje ya nchi na kuwazidi mataifa mengine, ili tuweze kufanikiwa tunahitaji wasanii wetu kushirikiana kuanzia wasanii wakubwa waliopata mafanikio ambao wamekuwa walimu na makocha wazuri kwa kuwapa ushauri wasaniii wadogo waweze kufanikiwa” alisema Waziri Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa ameahidi kusaidiana na kushirikiana na wadau wote wa Sanaa hatua inayosaidia wasanii walioibuliwa katika Bongo Star Search ili wasanii wote waweze kufanikiwa zaidi na kuvuka kwa pamoja katika maisha yao.   

Waziri Bashungwa amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa Sanaa na kuliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Chuo cha Sanaa na Utamaduni (TaSUBa) kushirikiana na mwendeshaji wa mashindano hayo Madam Ritha Polsen hatua itakayosaidia vijana hao kufanikiwa kimaisha kwa kunufaika na kazi zao za Sanaa huku akiahidi kushirikiana nao ili kuhakikisha wanafanikiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benchmark Production ambao ni waandaaji wa mashindano ya Bongo Star Search (BSS) Madam Madam Ritha Poulsen amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuthamini na kuipa kipaumbele sekta ya Sanaa nchini katika Serikali anayoiongoza.

Hatua hiyo imesaidia vijana na wadau wengine wa Sanaa kuendelea kufanya kazi zao za Sanaa wakiwemo waandaaji wa miswada, watenegenezaji wa kazi za Sanaa, wasanii wenyewe pamoja na taasisi zinazosimamia maslahi ya wasanii.

Mashindano BSS yalianza kwa kushirikisha vijana zaidi ya 200 kutoka mikoa yote nchini na kupekelea washindi watatu kupatikana ambapo Mshindi wa pili ni Zanael Kinyala kutoka Dar es salaam na mshindi wa tatu akiwa ni Petro Jairos kutoka Dodoma huku mwanamuziki kipenzi cha watazamaji na wasikilizaji wa mashindano hayo kupitia kisimbusi cha Star Times akiwa ni Alfredy Ally ambaye amezawadiwa runinga yenye ukubwa wa inchi 55 kutoka kampuni ya Star Times kwa matumizi yake
binafsi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post