NAIBU WAZIRI MABULA AWASHUKIA WAKURUGENZI HALMASHAURI KUZITELEKEZA IDARA ZA ARDHI


Na Munir Shemweta, WANMM KIBAHA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendelea ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu baadhi ya wakurugenzi wa halamashauri kwa kushindwa kuzihudumia idara za ardhi katika halmashauri zao na kuzifanya idara hizo kufanya kazi katika mazingira magumu.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, uongozi wa mkoa wa Pwani na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo tarehe 31 Desemba 2020 akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kukagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Pwani, Dkt Mabula alisema kuna baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wamekuwa wakorofi na kuziona idara za ardhi kama siyo sehemu ya idara zao na kuziacha bila kuzihudumia.

Alisema, baada ya kutoka waraka uliohamisha Maafisa Ardhi kurudi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuna baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri waliamua kujivua kuzihudumia idara hizo kwa kisingizio kuwa idara hizo sasa haziko chini yao na zimerejeshwa Wizarani.

Dkt Mabula alisema, waraka uliotolewa na kusambazwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa  ulieleza wazi kuwa wajibu wa Wizara ya Ardhi kwa watumishi wa sekta hiyo utakuwa kwenye  masuala ya sera, ajira na nidhamu lakini usimamizi utaendelea kubaki kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, majukumu ya kupanga miji ni ya halmashauri za miji , manispaa na majiji hivyo wakurugenzi wa halmashauri bado wana wajibu wa kuzihudumia idara hizo ili ziweze kupanga miji vizuri pamoja na kutoa huduma zinazohusiana na masuala ya ardhi.

‘’Hawa ni watumishi wenu kama walivyo wale wa idara nyingine za afya, elimu nk hivyo mnapaswa kuwahudumia vizuri ikiwemo kuwapatia vitendea kazi ili waweze kufanya kazi vizuri’’ alisema Dkt Mabula.

Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kubadilika na kuanza kuzihudumia idara za ardhi vizuri kwa kuzipangia idara hizo bajeti ya kutosha pamoja vitendea kazi kama magari na vifaa vya kupimia ili ziweze  kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akigeukia suala la ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi, Naibu Waziri Mabula aliwataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuziwezesha idara za ardhi ili ziweze kufuatilia madeni ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mkoa wa Pwani pekee unadai bilioni 32, 762,665,972 za kodi ya pango la ardhi kutoka kwa wadaiwa mbalimbali na kusisitiza kuwa kama  idara za ardhi zitawezeshwa vizuri zinaweza kukusanya mapato mengi  yatakayosaidia utekelezaji  miradi mbalimbali kama vile ya afya, elimu na miundombinu ukilinganisha na idara nyingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masamia alisema, pamoja na mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kukusanya kodi bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika suala hilo kutokana na hadi kufikia Desemba 31, 2020 ni Bilioni 61 ndizo zilizokusanywa na kutaka juhudi za makusanywa kuongezwa katika kila halmashauri. Malengo ya Wizara katika mwaka wa fedha 2020/2021 ni bilioni 200.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki uliopo wilayani Kibaha mkoani Pwani mradi unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Akiwa katika mradi wa ujenzi wa Ofisi hiyo , Dkt Mabula alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa miradi mbalimbali iliyokabidhiwa na kulitaka kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kujenga imani kwa wateja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post