WANANCHI KIJIJI CHA NYAGISYA WAZUIA MSAFARA WA MBUNGE WAITARA AONE WALIVYOJITOLEA KUJENGA ZAHANATI


Wananchi wa kijiji cha Nyagisya kata ya Kiore wakiongozana na mbunge Waitara kwenda kwenye ujenzi wa Zahanati baada ya kuzuia msafara wake
Wananchi wa kijiji cha Nyagisya kata ya Kiore wakiongozana na mbunge Waitara kwenda kwenye ujenzi wa Zahanati
Mbunge Waitara akiwasikiliza wananchi wa kijiji cha Nyagisya kwenye eneo wanakojenga zahanati ya kijiji
Mbunge Waitara akiwasikiliza wananchi wa kijiji cha Nyagisya kwenye eneo wanakojenga zahanati ya kijiji
***

Na Dinna Maningo,Tarime 
Wananchi wa kijiji cha Nyagisya kata ya Kiore jana wamesimamisha msafara wa mbunge wao wa jimbo la Tarime vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira Mwita Waitara kuendelea na safari wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa,wakimuomba kuongozana nao kwenda kuona namna wanakijiji walivyojitolea nguvu zao kuchimba msingi ili kujenga Zahanati.

Wananchi hao walikuwa wamesimama katikati ya barabara wakiwa wamebeba majembe,sululu,koreo,mabeseni vifaa walivyokuwa wakivitumia kuchimba msingi hali iliyomladhimu mbunge Waitara kushuka kutoka ndani ya gari pamoja na msafara wake ili kuwasikiliza wananchi ili ajue sababu ya kusimamisha msafara wake.

Wananchi hao walipaza sauti zao na kusema "Mbunge wetu Mbunge wetu tunaomba twende ukaone wananchi tulivyoamua kujitolea kujenga zahanati twendwe twende,hata hivyo Waitara akakubali kuongozana na wananchi kwa kutembea kwa miguu mwendo wa km.1 kwenda kushuhudia namna wananchi walivyojitolea katika ujenzi.

Baada ya Mbunge kutii wito wa kuongozana nao ,wananchi wakashangilia huku wakiimba na mkumsifu wakisema Waitara jembe Waitara Jembe Waitara ni Mwamba Waitara ni Mwamba hatukukosea kukuchagua...........

Walipofika katika ujenzi wananchi walimuonyesha mbunge matofali 3,500 waliyoyanunua kwa fedha zao na kuchimba msingi kwa nguvu zao hali iliyomfurahisha mbunge na kuwachangia shilingi milioni tano kwa ajili ya kununua mifuko ya Saruji kujenga Zahanati.

"Nawaomba watalaamu msaidie siyo ujenzi ukamilike alafu mnawaambia wabomoe kuwa ujenzi uko nchini ya kiwango,nawapongeza sana kwa uamuzi mzuri na mimi nachangia milioni tano ya saruji naombeni muendelee na moyo huo huo wa kuchangia", alisema.

Anna Wang'anyi alisema kuwa wameamua kujenga zahanati kwakuwa wamekuwa wakiteseka kutembea umbali mrefu zaidi ya km.2 kwenda kupata huduma ya zahanati ya Mtana iliyopo kata ya Manga na wengine wanapokosa nauli ya usafiri wa pikipiki kwenda hospitali ya wilaya ya Tarime ulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 5 kwa mgumu.

"Zahanati ikijengwa itatusaidia sana tukienda clinic zahanati ya Mtana Nesi wanatupa mabango eti si mjenge zahanati yenu ukienda hospitali ya wilaya unaambiwa hivyo hivyo wajawazito na watoto wanaopelekwa clinic wanateseka sana hali hii imesababisha wajawazito wengi kujifungulia nyumbani",alisema Wang'anyi.

Katarina Charles aliongeza"Ukienda Mtana kama ujauzito wako ni wa kwanza wanakwambia hawahudumii mimba ya kwanza  uende hospitali ya wilaya,ukijifungua unaombwa sh.10,000-20,000 tumefurahi sana kuanzisha zahanati hapa ni karibu,umbali umechangia baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha kwa kukosa huduma ya haraka",alisema Katarina.

Naibu Waziri huyo katika ziara yake aliongozana na maofisa wa Idara ya Elimu Halmashauri ya wilaya ya Tarime na viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tarime akiwemo Katibu wa CCM wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka,Katibu Mwenezi Wilaya Marema Sollo,Katibu vijana wilaya Newton Mwongi na Katibu Hamasa wilaya Remmy Mkapa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments