WANANCHI WA MBOPO WAMUOMBA RAIS MAGUFULI KUINGILIA MGOGORO WA ARDHI

 

Baadhi ya Wananchi wakimsilikiliza Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa Mbopo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza nao kwenye kikao chake alichokiitisha kwa wakazi wa maeneo hayo mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa Mbopo,Mohamed Bushir azingumza na Wananchi katika mkutano wa uliofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya ofisi ya Serikali ya mtaa Mbopo.Kinondoni jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Wananchi wakiwa na Mabango baada ya kudaiwa kupotezewa muda na mtu aliyedaiwa kuitwa kwa jina la Mgala,kwa kukosa kufika kwenye mkutano huo ambao yeye ulikuwa ukimuhusu pia.

****

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

 WAKAZI wa Wilaya ya Kinondoni, Mtaa wa Mbopo jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kuwasaidia kutafutia ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi uliopo kwenye eneo lao.

 Hii inatokana na kuwepo mtu anayetambuliwa kwa jina la Emmanuel Mgala amekuwa akidai eneo hilo ni la kwake huku akijua si kweli.

 Wakizungumza na mwandishi wetu, wakazi hao walisema wanaamini mgogoro huo utakoma iwapo Rais Magufuli ataingilia kati kwani kwa namna inavyoonekana mtu huyo hana woga na mara kadhaa amekuwa akikaidi wito wa viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mbopo, Mkoa wa Kinondoni.

 "Tunamuomba Rais Magufuli atusaidie, tunapata shida wakazi wa eneo hili, tunaomba utusaidie  hatuna makazi kwani haya makazi ambayo tunaishi sasa ni kama vile tumenyang'anywa na wenye fedha," alisema mkazi wa eneo hilo Fatuma Heri.

 Kwa upande wake Charles Kapuya amesema inasikitisha kuona ofisi ya Serikali ya Mtaa kila siku inamuita mtu mmoja lakini hataki kufika: "Serikali ya Mtaa inasema inamtambua mkazi huyo (Mgala) wakati mkazi mwenyewe hataki kuisikiliza Ofisi ya Serikali ya Mtaa ambayo ndio inamlinda. 

"Kwanza mimi nasikitika, niulize kitu kimoja kwa Serikali ya Mtaa, huyo Mgala ambaye anajiita ana mashamba, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa alikuja kwako kujitambulisha ana mashamba mangapi hapa Mbopo? Kama ana mashamba, je hayo mashamba analima nini? Je wananchi wako wananufaika nini na hayo mashamba au serikali inanufaika na kitu gani,” alihoji Kapuya na kuongeza:

 "Ni nani yeye aliyekuwa juu ya sheria kiasi cha kushindwa kuitii Ofisi ya Serikali ya Mtaa ambayo ndio yenye mamlaka, tuna mashaka na ofisi yako mwenyekiti wetu, unasema upo na wananchi leo hii mbele ya wananchi unawadanganya. Umetuambia hapa ulimuita Mgala mkazungumza naye, hatuhitaji mlizungumze nini na katika kikao hiki umempigia simu anasema hawezi kuja."

 Wakati huo huo, mkazi wa eneo hilo Tina Mfanga alisema kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbopo amekuwa akiwaita wananchi na kuwaambia wakutane na Mgala lakini amekuwa akikataa kufika.

 "Tupo hapa kwenye kikao anapigiwa simu hadharani anasema hawezi kuja ila atazungumza na Mwenyekiti," alisema Mfanga na kuongeza:

 "Vikitishwa vikao hatokei, kazi yake kupiga simu au atawasubirisha. Tunaomba tupewe majibu huyu ni mwananchi kama wananchi wengine au yeye ni tofauti na sisi, ndiyo maana wakati mwingine ofisi inamsikiliza sana yeye."

 Kwa upande wake Mselemu Athuman ambaye naye ni mkazi wa Mbopo alisema, Serikali iliamua kuja kuhakiki eneo hilo kwa lengo la kujiridhisha wapi ni makazi ya watu na wapi ni mashamba.

 "Kazi kubwa ni nyinyi viongozi wa Serikali za Mitaa kutambua hapa kuna mashamba au kuna makazi ya watu, hao wakazi mnaowakubali wanakaa wapi na hayo mashamba yako wapi," alisema Athumani.

 Akizungumza mbele ya wakazi hao, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbopo  Mohamed Bushir amewaambia aliamua kumuita Mgala ili kuzungumza na wananchi lakini amekataa.

 "Niliamua kumuita kwa kuamini hii ndio njia sahihi ya kupata ufumbuzi, lakini wananchi mmeona amekataa," alisema Bushir na kuongeza:

 "Nataka kuhakikishia tu si hapa Mbopo tu bali Mkoa wote wa Dar es Salaam kwa sasa mashamba hakuna.”.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments