MUME AUA MKE WAKE KWA KUMPIGA NGUMI NA MTWANGIO SHINYANGA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba (kulia), kushoto ni mfano wa kinu na mtwangio

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Mwanamke aitwaye Paulina Daudi (30) mkazi wa Mtaa wa Mageuzi kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga ameuawa kwa kupigwa ngumi na mchi wa kinu ‘mtwangio’ na mmewe aitwaye Samwel James baada ya kutokea ugomvi wa kifamilia.

Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba tukio hilo limetokeo Jumanne Januari 26,2021 majira ya saa tatu asubuhi na kutaja chanzo cha mauaji hayo kuwa ni ugomvi wa kifamilia.

“Paulina  Daudi (30) mkazi wa Mageuzi alishambuliwa kwa kupigwa ngumi na mchi mdogo ‘mtwangio’ sehemu mbalimbali za mwili wake na mume wake aitwaye Samwel  James akiwa nyumbani”,amesema Kamanda Magiligimba.

Ameeleza kuwa Paulina Daudi alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa Samwel James kwa kosa la mauaji kwani alikimbia mara baada ya tukio hilo.

Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa wanandoa kuacha mara moja tabia ya kuwashambulia wenza wao.

Aidha  amewasisitiza wanawake wote wanaofanyiwa vitendo vya ukatili mkoani shinyanga    wavunje ukimya,wafunguke ili matatizo yao ya kifamilia yaweze kushugulikiwa yakiwa katika hatua  za awali kabla madhara makubwa hayajatokea akibainisha kuwa vitendo vya ukatili  ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post