Jumla ya wanafunzi 759,706 sawa na asilimia 91.1 ya wanafunzi waliofaulu wakiwemo wavulana 368,174 na wasichana 391,532 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021.
Kauli hiyo imebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo wakati akitoa taarfa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021 leo jijini Dodoma.
Akizungumza Mhe. Jafo amesema kuwa kati ya wanafunzi 4,169 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni ambapo wanafunzi 970 watajiunga na shule za wanafunzi wenye ufaulu mzuri Zaidi.
Pia Mhe. Jafo amesema kuwa wanafunzi 1,238 watajiunga na shule za ufundi, wanafunzi 1,961 watajiunga na shule za bweni za kawaida.
Wanafunzi 755,537 wakiwemo wavulana 362,247 na wasichana 385,665 wamechaguliwa kujiunga na shule za Sekondari za kutwa katika maeneo mbali mbali nchini.
“Miongoni mwa waliochaguliwa, wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 2,491 wakiwemo wavulana 1,312 na wasichana 1,179 sawa na asilimia 75.0 ya wanafunzi wenye ulemavu waliofanya mtihani huo.
Mhe. Jafo ameeleza kuwa jumla ya mikoa tisa ya Kagera, Katavi, Lindi, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Songwe na Tabora imeweza kupangia shule wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.
Hata hivyo jumla ya wanafunzi 74,166 sawa na asilimia 8.9 wakiwemo wavulana 34,861 na wasichana 39,305 hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
“Hivyo wanafunzi wenye sifa ambao hawakupangiwa shule katika awamu hii ya kwanza watapangiwa shule katika awamu ya pili kabla ya tarehe 28 Februari, 2021”, ameeleza Mhe. Jafo
Kwa kuongezea Mhe. Jafo amesema kuwa wanafunzi hao wataendelea kupangiwa shule kadri Mikoa na Halmashauri zitakavyoendelea kukamilisha vyumba vya madarasa na madawati hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2021.
Aidha amewaagiza walimu na watendaji wa sekta ya Elimu katika ngazi zote kuongeza bidii katika usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu ili kufikia malengo ya elimu yaliyopangwa na serikali.
“Ninatoa wito kwa viongozi wa Mikoa na Halmashauri kushirikiana na wadau wa elimu kukamilisha majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza masomo yao mwezi Januari, 2021 bila vikwazo vya aina yoyote”, ametoa wito Mhe. Jafo.
Vile vile amesema kuwa wakuu wa mikoa na halmashuri kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni kwa wakati.
Mhe. Jafo amesema kuwa mzazi au mlezi ambaye atakuwa na hoja yoyote juu ya uchaguzi wa wanafunzi afike Ofisi za Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri husika ili aweze kuhudumiwa ipasavyo.
Aidha anaweza kupiga simu katika kituo cha huduma kwa wateja katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa namba ya simu 026-2160210 AU atume ujumbe mfupi wa (SMS) au WhatsApp kwa namba ya 0735160210
Tazama hapa Orodha ya Wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza Tanzania Bara kwa mwaka 2021.
CHAGUA MKOA ULIKOSOMA