MBUNGE JOSEPH MHAGAMA AFANYA ZIARA JIMBO LA MADABA.. AISHUKURU SERIKALI KUTOA FEDHA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA


Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Mhagama akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi za ndio Rais John Magufuli na Madiwani baada ya yeye kupita bila kupingwa.
 

Na Mwandishi wetu

Mbunge wa Jimbo la Madaba Mkoani Ruvuma, Joseph Mhagama ameishukuru serikali kwa kutoa Sh bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya   na jitihada inazofanya za kuimarisha huduma za afya katika jimbo hilo.

Mhagama alitoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano yake ya kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Alisema fedha hizo zinakwenda kuimarisha na kuboresha huduma za afya, hasa ikizingatia kuwa katika jimbo hilo hakuna hospitali kubwa ya wilaya.

Badala yake, wananchi wanategemea kupata matibabu katika zahanati na vituo vya afya vilivyopo.

Alisema wananchi wa Madaba, hawana budi kumshukuru Rais John Magufuli kwa kazi kubwa aliyowafanyia ya kupeleka maendeleo.

Alisisitiza kuwa heshima pekee, wanayoweza kumpa ni kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi inayobuniwa na kutekelezwa na serikali ili kuleta tija.

Alisema mbali na fedha za ujenzi wa hospitali ya wilaya, awali serikali ilitoa Sh milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya Madaba na Mtyangimbole, ambavyo vimeshakamilika na sasa wananchi wameanza kupata huduma za matibabu.

Alisema pia, serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) imeanza ukarabati wa barabara ya Madaba kwenda Ifinga Kata ya Matumbi  yenye urefu wa kilometa 48.

Wakati wa masika barabara hiyo ilikuwa haipitiki kwa urahisi, hivyo wananchi hushindwa kufanya shughuli za kujipatia kipato.

Mhagama aliwataka wananchi wa jimbo la Madaba kuwa wazalendo na kuiga mfano wa Rais John Magufuli wa kufanya kazi kwa kujituma ili kuondokana na hali ya umaskini na kuacha kuwa vibarua wa kufanya kazi katika mashamba ya watu kutoka nje.

Alitaka vijana kuacha kulalamika na kutumia muda wa kazi  vijiweni kucheza pool na kuwaachia wazee kuzalisha mali.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Theophanes Mlelwa alisema baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, kazi iliyobaki ni  madiwani na watendaji wa serikali,  kushirikiana kutatua kero na changamoto za wananchi ili kuharakisha maendeleo.

Mlelwa ambaye ni  diwani wa Wino aliwataka wananchi kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa uchaguzi na kuungana pamoja kuijenga Madaba, ambayo inahitaji  ushirikiano na umoja wa wananchi wote.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea, Nelly Duwe alisema chama kina imani kubwa na  mbunge Mhagama na diwani Mlelwa, kutokana na uchapakazi wao.

Aliwataka kutobweteka na mafanikio, baada ya kupita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post