![]() |
Mhe Neema Lugangira (Mb.) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani akitoa Mafunzo ya Lishe Bora kwa Madiwani Viti Maalum |
![]() |
Mwenyekiti wa UWT Mkoa Hajat Faiza kulia akichukua dondoo kwenye Mafunzo ya Lishe Bora na Madiwani Viti Maalum wa Mkoa wa Kagera |
MADIWANI wa Viti Maalumu wapatao 64 kutoka Mkoani Kagera
wamepatiwa mafunzo ya Lishe Bora kuhusu umuhimu wake na madhara yake
ikiwemo ya kiuchumi iwapo hawatazingatia .
Mafunzo
hayo yametolewa na Shirika la Agri Thamani yakiwa na lengo la
kuwaelimisha kwa kina madiwani hao wanawake kuhusu umuhimu wa lishe bora
kwa mama mjamzito, mama anaenyonyesha, mtoto chini ya miaka 5, kijana
balehe, wanaume na wazee n.k.
Aidha madiwani hao pia walipata uelewa pia juu ya
hali ya lishe nchini, madhara yake katika uzalishaji, jitihada kubwa
zinazofanywa na Serikali, malengo ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani
ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na wajibu wao kama viongozi.
Akizungumza
wakati wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Shirika la Agri Thamani, Mhe Neema
Lugangira (Mb) alisema kwamba baada ya mafunzo hayo wanategemea kuona
bajeti ya lishe ikiongezwa na kutolewa.
Alisema
bajeti hiyo itakapotolewa itumike kwa ajili ya afua za lishe
zinazokubalika na hilo linawezekana sababu Madiwani Viti Maalumu
wanashiriki vikao vinavyopitisha bajeti za Halmashauri na hivyo itakuwa
rahisi kwao kuweza kuitetea na kuifuatilia.
Kwa
upande wao Madiwani waliazimia kuanza na ajenda kuu tano ambazo ni
kujua hali za lishe za wilaya zao, utengaji wa bajeti ya lishe, kujua
aina za afua za lishe zinazokubalika, utendaji wa kamati za lishe na
utekelezaji wa mikataba ya lishe iliyosainiwa kati ya Mkuu wa Mkoa na
Wakuu wa Wilaya zao.
Post a Comment