KILIO KUOMBA SHULE ZA BWENI CHATAWALA MJADALA UCHAGUZI WA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA 2021 SINGIDA


Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Deogratius Yinza akiongoza  kikao cha Wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi wa Wanafunzi wanaotarajia kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2021 mkoani hapa jana.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Nelasi Mulungu, akizungumza.
Kikao kikiendelea.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka, akizungumza.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,  Edward Mpogolo akizungumza.
Wajumbe wakifuatilia kikao hicho.
Wajumbe wakifuatilia kikao hicho.
Wajumbe wakifuatilia kikao hicho.
Wajumbe wakifuatilia kikao hicho.
Kikao kikiendelea,
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kyaratu, akizungumza. 


                              

Na Godwin Myovela, Singida

 

WAJUMBE wa Kamati ya Uchaguzi wa Wanafunzi wanaotarajia kuingia kidato cha kwanza kwa mwaka 2021 mkoani hapa wameazimia, pamoja na mambo mengine, kuanza mara moja ujenzi wa shule za bweni walau moja kwa kila wilaya au halmashauri, lengo ni kupandisha kiwango cha ufaulu.

Suala lingine lililojitokeza katika kikao hicho ni kuwasihi wadau na wabunge wa maeneo husika kujitokeza kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula cha mchana kwa baadhi ya shule hususani vijijini kutokana na wazazi kukosa uwezo sambamba na jiografia ya maeneo husika kutokuwa rafiki.

Mjadala huo umefanyika leo, wakati wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi kidato cha kwanza 2021 kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kwa kuhusisha Katibu Tawala na Afisa Elimu Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Elimu ngazi mbalimbali na wadau wengine maalumu kutoka ndani ya halmashauri zote 7 mkoani hapa.

Pamoja na hivi karibuni serikali kuajiri walimu 314 lakini idadi hiyo imeonekana kuwa ni ndogo kuweza kukidhi msawazo wa ikama uliopo baina ya walimu na wanafunzi, mathalani mpaka sasa bado ni 1:78-150 hali inayozidisha wimbi la watoto wa shule za serikali kutofanya vizuri sana, ikilinganishwa na zile za binafsi.

Aidha, kupitia mjadala huo, baadhi ya maafisa utumishi waliombwa kujirekebisha na kuanza kuwajali, kuwa karibu zaidi, kuwapenda na kusikiliza shida za walimu na sio kutoa lugha chafu-ikiwemo kuwakatisha tamaa hasa pale wanapogubikwa na baadhi ya changamoto za kimaisha, suala ambalo nalo limeelezwa kuchagiza ufaulu kuwa hafifu kwa baadhi ya shule.

Huku baadhi ya wazazi nao wakinyooshewa vidole kwa kukataza watoto kuhudhuria masomo kwa kigezo cha kwenda kuchunga mifugo na shughuli nyingine, sanjari na kuwashawishi watoto wasifanye vizuri pindi wanapoingia kwenye mitihani yao ya kitaifa, hali inayozidi kuzorotesha kasi na juhudi za mkoa kufanya vizuri.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Nelasi Mulungu alikiambia kikao hicho kuwa kwa mwaka 2020 ufaulu katika Halmashauri 6 umeshuka isipokuwa halmashauri ya Manispaa ndio pekee ambao wameongeza ufaulu kwa asilimia 1.12,  na kuitaka kila halmashauri kujipanga na kuweka mikakati zaidi kwa ajili ya kuongeza ufaulu kwa mwaka 2021.

Mulungu akizungumzia hali ya ufaulu ndani ya mkoa kwa mwaka 2020, alisema  jumla ya wanafunzi  33,398  wakiwemo wavulana  15,727 na wasichana 17,671    walifanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi.  Kati ya wanafunzi hao waliofaulu ni 23,785  wakiwemo wavulana 11,116   na wasichana 12,669. Ufaulu huo ni sawa na asilimia 71.89, huku waliofeli ni wanafunzi 9,613 sawa na asilimia 28.78.

“Ufaulu wa mwaka huu 2020 ukilinganishwa na ule wa mwaka 2019 umeshuka  kwa asilimia 3.13, aidha, idadi ya wanafunzi waliofaulu imeongezeka kutoka wanafunzi 22,484 hadi 23,785,” alisema.

Akitoa tathmini ya matokeo hayo, Afisa Elimu huyo wa mkoa, alisema ufaulu kwa baadhi ya masomo umepanda na mengine kushuka ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2019. Mathalani, kwa somo la Kiswahili ufaulu umepanda kwa asilimia 0.80, huku somo la Kiingereza likishuka kwa asilimia 9.25,

Alisema Maarifa ya Jamii limepanda kwa asilimia 3.66, Hisabati limeshuka kwa asilimia 9.11, huku Sayansi nalo likishuka kwa asilimia 4.59.

Aidha, akizungumzia kuhusu ugawaji wa nafasi za Kutwa, Mulungu alibainisha kuwa ugawaji wa nafasi hizo umefanyika kufuatana na idadi ya wanafunzi waliofaulu katika ‘Catchment’ yaani shule zinazozunguka sekondari fulani, ikilinganishwa na idadi ya vyumba vya madarasa.  Hata hivyo, alisema jumla ya wanafunzi  23,726 wakiwemo Wavulana 14,423 na Wasichana  12,192 wamepata nafasi katika shule za Kata.

 

Kuhusu nafasi za Bweni, alisema Mkoa wa Singida umepatiwa nafasi 121 kwa aina ya bweni kawaida, bweni ufundi na ufaulu mzuri, ambapo nafasi za wavulana 78 na wasichana 43 kwa ajili ya wanafunzi hao watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani

Kwa mujibu wa Ofisi ya Afisa Elimu Mkoa, mpaka sasa jumla ya wanafunzi ambao hawajapata nafasi kwa chaguo la kwanza ni 524, na kati ya wanafunzi hao 488 wanatoka halmashauri ya Manyoni na Ikungi 36. Pamoja na mambo mengine sababu hiyo imeelezwa kuchangiwa na upungufu wa takribani vyumba 99 vya madarasa, ambavyo kwa agizo la serikali vinatakiwa viwe vimekamilika kabla ya Februari 28, 2021.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post