DOKTA MPANGO AWAPA WATENDAJI TAASISI ZA UMMA SIKU 9 KUJIELEZA


Na Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ametoa muda wa siku 9 kuanzia 22 hadi 31 Desemba 2020 kwa Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma  kujieleza kwa maandishi sababu zilizozifanya taasisi zao kuchangia mfuko mkuu wa Serikali chini ya kiwango, kutochangia huduma za jamii pamoja na kutozingatia ukomo wa matumizi ya asilimia 60 ya mapato ghafi ya taasisi na mashirika yao kwa mujibu wa Sheria.

Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma alipokutana na Wakuu wa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma 236 kutoka nchi nzima ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake ya kikazi na taasisi mbalimbali za Serikali ili kutoa mwelekeo mpya wa utendaji wa taasisi hizo hususan kuimarisha na kuongeza mapato ya Serikali.

“Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali bado hauridhishi. Kwa mwaka 2019/20, mchango wa Taasisi na Mashirika ya Umma katika pato la Taifa ulikua chini ya asilimia moja (1%), kiwango hiki ni kidogo sana ikilinganishwa na uwekezaji wa Serikali katika Taasisi na Mashirika haya” Alisema Dkt. Mpango

Alimwagiza Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka kuhakikisha taarifa hiyo ya maandishi kutoka kwa wakuu hao wa Taasisi inamfikia tarehe 31 Desemba 2020 na kutangaza kufuta likizo za sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa Viongozi hao ili watekeleze maelekezo yake.

Alifafanua kuwa Kifungu cha 47 cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 na kifungu cha 8 cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 iliyorekebishwa mwaka 2015, kinazitaka Taasisi na Mashirika ya Umma kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali lakini bado kuna Taasisi ambazo zinachangia chini ya kiwango kilichowekwa kisheria na zipo Taasisi na Mashirika hata mchango kwa jamii (CSR) hawatoi kabisa!

Dkt. Mpango alisema kuwa Kifungu cha 46 (1) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 na Kifungu cha 10A cha Sheria ya Msajili wa Hazina iliyorekebishwa mwaka 2015, kinaweka ukomo wa gharama za uendeshaji kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yasiyo ya kibiashara kutozidi asilimia 60 ya mapato ya ghafi lakini bado kuna Taasisi na Mashirika ya Umma zinavunja sheria hiyo.

“Kifungu 46 (2) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015 kinaelekeza Taasisi na Mashirika ya Umma kuwasilisha asilimia sabini (70) ya ziada kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali baada ya kuondoa gharama za mishahara na kuzingatia ukomo wa matumizi ya uendeshaji uliotajwa kwenye aya 2.1(b) lakini yapo mashirika na Taasisi hayatekelezi matakwa haya” alisisitiza Dkt. Mpango

Aliwaagiza wakuu hao wa Taasisi kuhakikisha kuwa wanapunguza matumizi yasiyo na tija na yasiyo ya lazima ikiwemo misafara mikubwa ya watendaji na wajumbe wa bodi kutembelea miradi ili kuziwezesha taasisi zao kuwa na fedha za kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi mikubwa ya kijamii na ya kimkakati inayotekelezwa nchini.

“Serikali chini ya uongozi shupavu wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kielelezo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa umeme (MW 2115) Mto Rufiji, uboreshaji wa usafiri wa anga na majini, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, Elimu bila ada, usambazaji wa umeme vijiji vyote nchini, na uboreshaji wa huduma za afya na maji” Alifafanua Dkt. Mpango

Alisema Idara zote zinazokusanya maduhuli, na Halmashauri zote lazima zifanye jitihada kubwa zaidi kuongeza ukusanyaji wa  mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuwezesha kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha za ndani kwa kiwango kikubwa na kwamba mambo hayo yatafanikiwa endapo watendaji hao wataacha kufanyakazi kwa mazoea.

Aidha, Dkt. Mpango alimpongeza Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka kwa Kusimamia na kuwezesha urejeshwaji wa mali za Serikali, kupitia Kamati Maalum ya Uhakiki wa Mali za Serikali, ambazo zilikuwa zinamilikiwa na watu binafsi bila kufuata sheria na taratibu.

“Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2020, jumla ya mali zisizohamishika 1,562 zilibainika kushikiliwa au kumilikiwa kinyume cha sheria kwenye mikoa 19 kati ya 26 iliyohakikiwa. Mali hizo zinajumuisha nyumba/majengo (862), viwanja (559), mashamba (43), kampuni (2) na maghala (96)” Alifafanua Dkt. Mpango

Alisema mali hizo za Serikali zilikuwa zinamilikiwa na baadhi ya watu wasio waaminifu bila kuwa na hofu na kwamba zoezi la kutambua na kurejesha mali za Serikali zilizoko kwenye mikono isiyohusika ni endelevu.

Aliipongeza pia Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia Taasisi na Mashirika ambayo ilisababisha kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka shilingi bilioni  161 mwaka 2014/15 hadi kufikia shilingi bilioni 983  mwaka 2019/20, ikiwa ni ongezeko la asilimia 510.

Dkt. Mpango aliziagiza Taasisi zote za umma zihakikishe zinajiunga na mifumo ya kukusanya mapato ya Serikali (GePG), mfumo wa matumizi ya fedha za Serikali (MUSE) pamoja na mifumo mingine ya uandaaji na usimamizi wa bajeti ili kuongeza ufanisi na madhibiti matumizi yasiyosahihi ya fedha za Serikali.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Bi. Mwaidi Alis Khamis aliwataka watendaji hao kujiepusha na vitendo vya ukiukaji wa maadili ikiwemo rushwa na matumizi mabaya ya Serikali na kuonya kuwa yeye na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango hawatavumilia vitendo hivyo.

Alisema kuwa Serikali inamatarajio makubwa na viongozi hao ili kuhakikisha kuwa wananchi masikini wanaondokana na hali hiyo kwa kuboresha maisha yao na kwamba mambo hayo yatawezekana kutokana na utendaji kazi wao mzuri ikiwemo kukusanya ipasavyo mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Athumani Mbuttuka, alimhakikishia Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwamba maelekezo aliyoyatoa yatafanyiwa kazi na kuwaagiza wakuu hao wa Taasisi kusimamia ipasavyo maelekezo hayo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post