ASKARI POLISI ASIMULIA JINSI ALIVYOPIGWA NA MUMEWE


Askari Polisi Juliana Kwayi, akionesha jeraha usoni alilosababishiwa na mume wake.
***
Askari wa Jeshi la polisi mkoani Mwanza, Juliana Kwayi, ameamua kuvunja ukimya na kuviomba vyombo vya dola kumchukulia hatua za kisheria mume wake anayefahamika kwa jina la Nicolus Laurent, kufuatia mwanaume huyo kuwa na tabia ya kumpiga mara kwa mara na kumsababishia majeraha.

Askari huyo anayefanya kazi katika kituo cha polisi Nyamagana mkoani Mwanza, amesema kwa kipindi cha miaka minne toka alipofunga ndoa na mwanaume huyo, amekuwa akiambulia kipigo kutoka kwa mwanaume huyo ambaye ni Meneja Msaidizi wa shule za Musabe, huku chanzo kikubwa cha hayo ni mgogoro walionao.

"Nilijeruhiwa na mume wangu kutokana na mgogoro uliopo mahakamani wa kudai talaka na tugawane mali tulizonazo, alikuja nyumbani akaniambia nataka uondoke humu ndani baadaye akaanza kunipiga na kuanza kusema bora niende jela kuliko wewe kubaki kwenye hii nyumba, alinijeruhi na nilipoenda hospitali nikashonwa nyuzi nane naomba tu sheria ifuate mkondo wake", amesimulia Juliana.

Aidha mwanaume huyo Nicolus Laurent, akihojiwa na EATV hakujibu chochote.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, amesema kuwa hakuwahi kupata taarifa kutoka kwa Askari huyo kama anapitia manyanyaso hayo na kuongeza kuwa hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria na Askari akifanyiwa kitendo chochote cha kinyama, sheria zitachukuliwa kama ambavyo wanavyosimamia sheria kwa mtu mwingine yeyote.

Chanzo - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post