DK. BASHIRU AWAKARIBISHA CCM WANAWAKE IMARA WA UPINZANI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ali, amesema chama chake kinawakaribisha wanasiasa wanawake ‘shoka’ wa upinzani watakao hitaji kujiunga na chama hicho.
Dk. Bashiru aliyasema hayo jana jijini hapa, wakati alipokuwa akifungua semina ya siku mbili kwa sekretarieti ya CCM na kamati za utekelezaji za jumuiya tatu za chama hicho.

Alisema katika uchaguzi mkuu 2020, wanawake kutoka vyama vya upinzani pamoja na wa CCM, wameonyesha ushindani mkubwa wa kisiasa hali iliyoonyesha walivyo na uwezo mkubwa wa uongozi.

“Mwaka huu tumeona nguvu ya kinamama wa upinzani na hata ndani ya CCM, katika kupambana kwenye nafasi za ubunge haijalishi wapo katika chama kikubwa au kidogo cha siasa kutokana na hali hii napenda kuwaambia kinamama wa vyama vya upinzani majembe wenye uwezo karibuni CCM,” alisema Dk. Bashiru.

Kadhalika, alisema kutokana na wanasiasa wanawake kuwagaragaza wagombea wa ubunge wanaume katika uchaguzi mkuu 2020, inamaanisha kuwa wana uwezo mkubwa ambao chama kinatakiwa kuutumia.

“Kama yule mbunge mwanamama wa CHADEMA aliyemshinda Kessy (Ally) kule Jimbo la Nkasi Kaskazini, pale kumtoa Kessy siyo jambo jepesi inatakiwa mtu mwenye uwezo, lakini pale Mbeya Mjini kwa Naibu Spika, hali hii inamaanisha kuwa kinamama wanastahili kupelekwa kwenye majimbo magumu ili kuyarejesha,” alisema Dk. Bashiru.

Aliziagiza jumuiya za CCM kufanya uchunguzi na tathmini ya kina kubaini mamluki na maadui waliokihujumu chama wakati wa uchaguzi mkuu, Oktoba 28, mwaka huu.

Dk. Bashiru alisema uchaguzi huo umeweka historia ya aina yake katika demokrasia za vyama vingi nchini ambao umeonyesha dhahiri maadui wa nchi na marafiki wa kweli kupitia mijadala na hoja mbalimbali zilizoibuka.

Alisema ushindi uliopatikana ni matokeo ya uchapakazi wa jumuiya zote kupitia mabalozi wa CCM zaidi ya 250,000 ambao ndio wenyeviti wa mashina ya chama.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments