MOTO WAUNGUZA NYUMBA NA KUUA MTOTO SIMIYU


Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu ACP Richard Abwao

Na Mwandishi wa Malunde 1 blog - Bariadi 
Mtoto aliyejulikana kwa jina la Philimon Matege mwenye umri wa miaka miwili mkazi wa Kijiji cha Ibulyu kata ya Sakwe wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu amefariki dunia akiwa chumbani baada ya moto kuunguza nyumba. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu ACP Richard Abwao amesema tukio hilo limetokea jana Jumatatu Oktoba 11,2020 majira ya saa moja na nusu usiku katika kijiji cha Ibulyu, kata ya Sakwe wilayani Bariadi. 

“Nyumba ya Liku Juma (20) mkazi wa Ibulyu iliungua moto na kusababisha kifo cha Philimon Matege mwenye umri wa miaka 2, aliyekuwa ndani ya nyumba hiyo”,amesema Kamanda Abwao. 

Amesema chanzo cha moto bado kinachunguzwa na kwamba hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. 

Ameongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Mji wa Bariadi kwa ajili ya uchunguzi wa daktari.

Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika matumizi ya vifaa mbalimbali ili kujikinga na majanga ya moto. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments