RC TELACK AONYA WANAOPANGA KUFANYA VURUGU SIKU YA UCHAGUZI... 'PIGA KURA RUDI NYUMBANI..ACHANA NA HABARI ZA KULINDA KURA'

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24,2020.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack amesema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28,2020 unakuwa salama huku akiwaonya baadhi ya watu wanaopanga kufanya vurugu kuachana na mipango hiyo.

Telack ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Shinyanga ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 24,2020 wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake ambapo pia amewatahadharisha vijana kuepuka kutumiwa na wanasiasa kuharibu amani ya nchi.

“Ninawaomba sana wananchi wa mkoa wa Shinyanga wenye sifa ya kupiga kura wajitokeze kwenda kupiga kura Oktoba 28,2020 ili wachague viongozi wale wanaona wanaweza kuendesha nchi yetu.

Muda wa kupiga kura utaanza saa moja asubuhi mpaka saa 10 jioni,niwasihi wananchi wawahi kwenye vituo vya kupigia kura ili kuepuka msongamano usio wa lazima. Baada ya kupiga kura wananchi warudi majumbani wakaendelee na shughuli zao kama kawaida”,amesema Telack.

“Niwasihi sana vijana wetu wasitumike kujaribu kuharibu amani yetu kwa namna yoyote,tupige kura turudi majumbani mwetu kuendelea na shughuli zingine, matokeo yatatangazwa na Tume ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria .Kila kituo kitakuwa na Mawakala wa vyama vya siasa hivyo hakuna atakayeiba kura, achaneni na mambo ya kusema mnakaa vituoni kulinda kura. ”,ameongeza Telack

Mkuu huyo wa mkoa amesema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba watu wote wanaotaka kwenda kupiga kura,wanapiga kura na shughuli zote za kijamii zinaendelea bila kuathiriwa na kitu chochote.

“Naomba kuwahakikishia wananchi wote wa Shinyanga kuwa usalama utakuwepo wa kutosha kwa hiyo asiwepo mtu yeyote ambaye atajaribu kwa namna yoyote kuzuia wananchi wasiende kupiga kura. Wewe ukiona mtu anazunguka barabarani anajaribu kukuzuia wala usirudi nyuma kwa sababu usalama utakuwepo wa kutosha”, ameeleza Mkuu huyo wa mkoa.

Amewasihi wale wote wanaodhani wamejiandaa kufanya fujo yoyote siku ya uchaguzi waache kwa sababu serikali imejiandaa vizuri kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama.

“Napenda kuwafahamisha kuwa yapo maisha baada ya uchaguzi, Hii Tanzania ni ya kwetu,tuilinde kwa nguvu zetu zote na tusijaribu na asijaribu mtu yeyote kufanya vitendo vya uvunjivu wa amani”,amesema. 

Katika hatua nyingine amevitaka Vyombo vya habari na waandishi wa habari kutotangaza matokeo ya uchaguzi akidai kuwa wenye mamlaka ya kutangaza matokeo ya uchaguzi ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Waandishi wa habari msitangaze matokeo ya uchaguzi kwa mhemko wowote. Sasa usianze sijui watu wanajumlisha matokeo ya kata na wewe unaanza kutoa matokeo,  Hapana. Kuweni Neutral kwenye jambo hili la uchaguzi. Msikubali kutumika ili thamani ya kazi zenu iendelee kubaki kwani kuna maisha baada ya uchaguzi”,amesema Telack.

Kwa upande wake, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga amesema maandalizi ya uchaguzi yamekamilika na kwamba jumla ya vituo vya kupigia kura mkoani Shinyanga vitakuwa 2700.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake na kuhamasisha wananchi wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura  Oktoba 28,2020. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Zainab Telack akiwasihi waandishi wa habari kuepuka kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa mihemko badala yake wasubiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi itangaze matokeo.
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga.
Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga akizungumza na  waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu 2020.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments