VIONGOZI WA DINI WA KAMATI YA AMANI WAKEMEA MADHABAHU KUTUMIKA KISIASA

Kamati ya Amani ya Viongozi wa dini Mkoa wa Dar es Salaam imewaomba viongozi wa dini nchini kuacha kutumia nyumba za ibada kama majukwaa ya siasa kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha amani ya nchi.


Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum ambaye amesema kuwa, baadhi ya viongozi wa dini wameanza tabia ya kuwanadi wagombea katika nyumba za ibada jambo ambalo halitakiwi kufanyika na kupelekea kuvunja amani ya nchi.

Amesema, kitendo hicho kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa dini kinaweza kupelekea kuvuruga amani iliyopo na kupelekea kuweka matabaka.

Sheikh Salum amesema, kazi kubwa ya viongozi wa dini ni kuhubiri amani na si kusimama katika nyumba za ibada na kuaza kufanya kampeni kwani si jukwaa sahihi.

“Sisi kwa umoja wetu viongozi wa dini wote wa kamati za amani na kwa ujumla wake hatupendezwi na tabia iliyoanza kujitokeza kwa sasa ya kuona maaskofu, mashekhe, Mapadri maimamu wanasimama katika nyumba za ibada kufanya kampeni na kumnadi Mgombea yoyote kufanya hivi ni kuatarisha amani ya nchi yetu”amesema Sheikh Salumu

Amesisitiza kuwa, nyumba za ibada zikianza kufanya kampeni zitakuwa zimepola nafasi za wanasiasa na majukwaa yao.

Amesema, watanzania wanapaswa kuachwa waende katika majukwaa ya siasa wakasikilize sera za wagombea ili waweze kuchagua ni nani anawatosha na kuwataka viongozi wa dini kutokutumiwa na wanasiasa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post