PINDA AZINDUA KAMPENI ZA CCM BABATI MJINI, AMNADI GEKUL

Na John Walter-Babati

Mlezi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara, Waziri mkuu mstaafu wa awamu ya nne Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda amewataka watanzania waendelee kukiamini chama hicho kwa kuwapigia kura Madiwani,Wabunge na Rais ifikapo Oktoba 28,2020.

Ameyazungumza hayo Mjini  Babati  wakati akimnadi kwa wananchi wa mji huo  mgombea ubunge Paulina Gekul katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Papaa.

Amesema Chama cha mapinduzi ni chama Kikongwe  na kimefanya mambo mengi hivyo ni vigumu kuondolewa madarakani kwa kuwa kimejidhatiti   kujali maslahi ya watu na utekelezaji wa kile wanachokiahidi.

Amesema yote hayo yanafanyika katika mazingira ambayo ni tunu kwa Watanzania wote wa Bara na Zanzibar katika hali ya amani na Utulivu ambavyo ni tunu kubwa tangu kupatikana kwa uhuru na kwamba hakuna M'badala wake zaidi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Pinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020,  ni Mratibu  wa kamati za Kampeni  katika mikoa ya Manyara,Arusha,Kilimanjaro na Tanga.

Mgombea Ubunge Paulina Gekul amesema serikali imefanya mengi katika Jimbo la Babati na kata zake nane kwa kuleta maendeleo katika nyanja zote ikiwemo Elimu,Afya na Miundo mbinu.

Amesema kupitia Serikali ya  Chama cha Mapinduzi Jimbo hilo kata zote zinapitika kwa kuwa bara bara zote zimechongwa na TARURA na kamba katika kipindi kijacho cha awamu ya pili,   wanatarajia kupokea mradi mwingine wa lami zaidi ya kilomita 35 ambazo zitaondoa vumbi katika mji huo.

Gekul amesema katika kukamilisha ujenzi wa Miundo mbinu ya Mitaro na Vivuko katika mji wa Babati, wanajiandaa kupokea zaidi ya shilingi Bilioni 10.4 ili kukabiliana na Mafuriko.

Akizungumzia Mawasiliano, Gekul amesema serikali kupitia mtandao wa Halotel wanajenga Minara ili vijiji vya Imbilili,Himiti,Chem Chem vilivyokuwa havipati mawasiliano viweze kunufaika.

Kuhusu Ujenzi wa Kituo kikuu cha Mabasi, Mgombea huyo amesema katika awamu ya pili kuanzia mwezi Machi,2021  serikali imetenga  Bajeti ya Shilingi Bilioni 12.7 kwa ajili ya miradi ya Kimkakati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527