MAJALIWA: CCM HAIKURUPUKI


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Chama Cha Mapinduzi hakikurupuki katika kuiwekea malengo Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Amesema CCM imekuwa ikiielekeza Serikali kutekeleza shughuli za maendeleo kupitia ilani ya uchaguzi ambayo imesheheni mambo yote ikiwemo miradi mbalimbali kama vile ya afya, maji, elimu na miundombinu.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Septemba 3, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Polisi wilayani Longido mkoani Arusha wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Longido Dkt Stephen Kiluswa.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli na sasa imeandaa ilani nyingine ya 2020-2025 ambayo nayo imeweka msisitizo katika masuala mbalimbali ikiwemo uboreshwaji wa huduma za jamii.

Pia, alisema msisitizo mwingine uliowekwa katika ilani hiyo ni kuilekeza Serikali iendelee kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, kukuza uchumi na aliwasihi wananchi kuhakikisha wanampigia kura nyingi Rais Dkt. Magufuli ili aweze kuendeleza kazi kubwa aliyoanza ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumzia sekta ya mifugo, Mheshimiwa Majaliwa alisema sekta hiyo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi hivyo Serikali itaendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na tayari kiwanda kikubwa cha kuchakata bidhaa za mifugo kimejengwa Namanga, wilayani Longido.

Alisema kiwanda hicho kinauwezo wa kuchakata ng’ombe 300 hadi 500 kwa siku, mbuzi na kondoo 3,000 hadi 4,000 kwa siku na kinatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 300. Kiwanda hicho kinatarajiwa kuanza uzalishaji Septemba, 2020, amewataka wanaLongido kuendelea kuiamini CCM.

“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2015 hadi 2020 Chama Cha Mapinduzi kilijielekeza katika kuhakikisha sekta ya ufugaji inaimarishwa ili kuwawezesha wananchi kunufaika na ukuaji wa sekta hiyo na mafanikio tumeyaona.”

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM wa mkoa wa Arusha na wilaya ya Longido, wagombea wa nafasi ya ubunge kwa tiketi ya CCM wa majimbo yote ya mkoa wa Arusha na wagombea wa udiwani wa Kata 18 za wilaya ya Longido ambao wote wamepita bila kupingwa.

Wengi ni pamoja na viongozi wa kimila wa kabila ya Kimasai ambao waliweka msimamo wa kuhakikisha wanamchagua Rais Dkt. Magufuli pamoja na mgombea wa ubunge Dkt. Kiluswa kutokana na kuridhishwa na utekelezaji wa shughuli za maendeleo zilizofanyika nchini ikiwemo na wilaya ya Longido.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post